• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Ajabu ya Mutua kumshtaki Ruto kwa Raila

Ajabu ya Mutua kumshtaki Ruto kwa Raila

Na LEONARD ONYANGO

GAVANA wa Machakos, Dkt Alfred Mutua, amefichua jinsi alivyomshtaki Naibu Rais kwa Kiongozi wa ODM Raila Odinga, akidai kwamba alitishiwa maisha na Dkt William Ruto.

Alipoenda kupiga ripoti jana kwa polisi akitaka wamchunguze na kumkamata Naibu Rais, ilifichuka alikuwa amemkimbilia Bw Odinga siku ambapo anadai alitishiwa maisha na Dkt Ruto katika Ikulu ya Nairobi.

Kupitia taarifa aliyoandikisha katika Kituo cha Polisi cha Kilimani jijini Nairobi, Dkt Mutua alisema Bw Odinga alikuwa amesimama karibu tukio hilo lilipotendeka wakati wa maankuli ya jioni kwa heshima ya Waziri Mkuu wa Barbados, Mia Motley, wiki iliyopita.

Kulingana na taarifa hiyo, Gavana huyo wa Machakos aliwaambia polisi kuwa alienda kumsalimia Dkt Ruto, lakini Naibu Rais alishikilia mkono wake kwa nguvu na kumwambia: “Wewe jamaa umekuwa ukinichapa sana. Wewe lazima nikugonge. Nitakugonga.”

Dkt Mutua alidai kuwa baadaye Dkt Ruto alimsukuma kando na kumnyooshea kidole huku akimwambia: “Wewe ngoja utaona, tumekuonya.”

“Nilijawa na hofu sana baada ya Dkt Ruto kunikodolea macho na kunitolea sauti ya ukali,” akaelezea Dkt Mutua katika taarifa yake kwa polisi.

“Baada ya kutishiwa na Dkt Ruto nilienda kwa Bw Odinga nikamwelezea. Baadaye nilielezea maafisa wengine wa ngazi ya juu serikalini,” akaongeza.

Sasa gavana huyo anamtaka Inspekta Jenerali wa Polisi, Hillary Mutyambai kumwongezea walinzi.

Kando na Dkt Ruto, gavana huyo aliripoti kuwa pia Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale na mwenzake wa Seneti Kipchumba Murkomen walimtisha.

Kulingana na Dkt Mutua, wawili hao walimtishia maisha mnamo Novemba 25, mwaka huu, katika Ikulu ya Nairobi wakati Jopokazi la Maridhiano (BBI) lilipowasilisha ripoti yake kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Anadai Bw Murkomen aliapa ‘kumgonga’ kutokana na mazoea yake ya kutoa kauli za kupinga Dkt Ruto.

Hata hivyo, wawili hao jana walimpuuzilia mbali Dkt Mutua na kumkejeli wakisema amezoea vioja na hakuna mtu ana muda wa kumtolea vitisho aina yoyote.

“Tumezoea Mutua kwa kuandika michezo ya kuigiza. Nani anaweza kutishia Mutua? ana ushawishi gani wa kisiasa?” akauliza Bw Murkomen.

Naibu Rais alikuwa hajajibu madai hayo kufikia wakati wa gazeti hili kuchapishwa jana.

Dkt Mutua anaamini matukio hayo yametokana na jinsi amekuwa akipinga misimamo ya Dkt Ruto na kikundi cha Tangatanga.

Ripoti hiyo ya Gavana Mutua ilizua msisimko katika mitandao ya kijamii.

Watumizi wengi wa mitandao ya kijamii walimkejeli na kudai anajitafutia umaarufu kwa kila njia.

You can share this post!

Sakaja sasa amezea mate kiti cha Sonko

Operesheni kali barabarani msimu wa sherehe ukianza

adminleo