Operesheni kali barabarani msimu wa sherehe ukianza
JOHN NJOROGE na STANLEY NGOTHO
POLISI wameanzisha msako mkali dhidi ya ukiukaji sheria za barabarani msimu huu wa sherehe za Krismasi.
Mjini, Molo walinasa magari zaidi ya 60 katika kizuizi cha Mau-Summit, barabara ya Molo-Kericho.Operesheni hiyo iliongozwa na naibu mkurugenzi wa NTSA Cosmas Ngeso, maafisa wa polisi kutoka Nairobi na maafisa wengine kutoka eneo hilo.
Mkuu wa Trafiki katika eneo la Mau Summit Nixon Kitur alisema maafisa wamekagua magari yote hasa vidhibiti mwendo, mishipi, leseni, magari mabovu yasiyostahili kuwa barabarani miongoni mwa sehemu zingine zinazostahili.
‘Madereva wachache ndio hawajazingatia sheria za barabara ikilinganishwa na mwaka uliopita. Wale ambao hawajazingatia na kuyatengeneza magari yao watafikishwa mahakamani,’ akasema Bw Kitur.
Alisema operesheni hiyo itaendelea hadi sehemu zingine kama vile Londiani katika barabara kuu ya Kericho-Kisumu hadi Kisumu ili kuhakikisha usalama barabarani umeimarishwa.
Naye msimamizi wa Trafiki mjini Molo Moses Nderitu alisema polisi wana vifaa vya kutosha vya kupima madereva ambao watalewa na kuendesha magari wakati wa msimu huo.
Katika barabara ya Nairobi-Mombasa, mamia ya wasafiri walikwama kufuatia msako katika eneo la Athi River, Kaunti ya Machakos. Magari yasiyopungua 75 ya uchukuzi wa umma yalinaswa katika msako huo ulioanza alfajiri ukilenga zaidi magari ya kusafiri masafa marefu.
Mabasi kadhaa yaliyokuwa yakielekea au kutoka Mombasa yalinaswa kwa ukiukaji sheria za barabarani.
Wasafiri waliokuwa wameandamana na watoto wao ndio walioathiriwa zaidi. Wengine walilazimika kuabiri magari mengine ili kuendeleza safari na kulipa nauli zaidi.Ingawa kuna waliosikitishwa na hali hiyo, wengine walisema hawaezi kulalamika kwani kuna umuhimu kuzuia ajali za barabarani.
Kamanda wa polisi katika Kaunti ya Machakos, Bw Karanja Muiruri ambaye aliongoza operesheni hiyo alisema wengi walionaswa walipatikana wakiendesha magari yasiyostahili kuwa barabarani, wengine wakakamatwa kwa kuendesha magari kwa kasi ya juu kwani walivuruga mitambo ya kudhibiti mwendo.
Alisema iligunduliwa madereva wengi wanataka kufika wanakoenda haraka ili wabebe safari nyingi zaidi ya ilivyo kawaida kwani wasafiri wameongezeka mno msimu huu wa sikukuu za Krismasi.