• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:55 PM
Mvua sasa kupungua siku 7 zijazo

Mvua sasa kupungua siku 7 zijazo

NA COLLINS OMULO

IDARA ya utabiri wa hali ya hewa imetangaza kwamba mvua kubwa ambayo imekuwa ikishuhudiwa maeneo mengi nchini itapungua sana katika kipindi cha siku saba zijazo.

Tangazo hilo limetolewa huku ikikisiwa kuwa zaidi ya watu 100 wameaga dunia baada ya kusombwa na maji ya mafuriko, maelfu wakilazimika kuhama makazi yao na mali yao kuharibiwa.

Eneo la Kaskazini Mashariki ndilo liliathirika vibaya na mvua hiyo ambayo ilianza kunyesha mwanzo wa Novemba hadi wiki ya kwanza ya mwezi Disemba.

Hata hivyo, idara ya hali ya hewa sasa inasema eneo hilo litasalia kame huku mvua ya kiwango cha kadri ikishuhudiwa Kusini mwa Kenya.

“Mvua inatarajiwa kupungua katika maeneo mengi nchini katika muda wa siku saba zijazo. Hata hivyo, mvua kubwa itanayesha Disemba 21 katika maeneo ya Kati, Kusini Mashariki, Kusini Magharibi na maeneo ya Pwani,” akasema Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Idara ya utabiri wa hali ya hewa Bernard Chanzu.

Afisa huyo aliongeza kwamba mvua imekuwa ikipungua maeneo mbalimbali ya nchi tangu mwanzo wa mwezi huu wa Disemba.

Kulingana na idara hiyo, jua kali litawaka katika kaunti za Turkana, Pokot Magharibi na Samburu asubuhi na mchana kati ya Disemba 17 na Disemba 23.

Hata hivyo, jua litashuhudiwa asubuhi kisha mvua ya kadri katika Kaunti za Magharibi na Bonde la Ufa huku jua likiangaza asubuhi na jioni jijini Nairobi na maeneo jirani.

You can share this post!

Waathiriwa wa ghasia za 2007 walia kukosa fidia sikukuu...

Rais wa zamani wa Pakistan ahukumiwa kifo

adminleo