NGILA: Sharti sote tuheshimu sheria ya kulinda data
NA FAUSTINE NGILA
DATA za kibinafsi zimekuwa dhahabu kwa kampuni nyingi katika kujiendeleza kiuchumi, hasa katika enzi hii ya mageuzi ya kidijitali.
Katika miaka michache iliyopita, tumeshuhudia taarifa nyingi za siri za Wakenya zikikusanywa, kuchambuliwa na kuuzwa kwa manufaa ya kampuni za matangazo nchini na kimataifa.
Ni mtindo huu ambao ulichangia serikali kuamua kudhibiti usambazaji wa data za siri bila idhini ya Wakenya, na kubuni Sheria ya Ulinzi wa Data iliyotiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta hapo Novemba 8, 2019.
Ninaelewa fika matumizi ya data za kibinafsi katika kukuza sekta ya fedha ambapo data kuhusu maisha ya wananachi huchambuliwa na kutumiwa kutoa maamuzi ya kukopesha hela, kutoa huduma za bima na kutangaza bidhaa za kampuni mbalimbali kupitia kwa arafa za simu.
Uwepo wa pengo kubwa la matumizi ya data bila kujali sasa umeisha, na kampuni yoyote inayotaka kutumia data kufanya biashara itatakiwa kuomba idhini ya wanaotoa taarifa zao, na kueleza jinsi data hiyo itatumika.
Chini ya sheria hiyo mpya, Wakenya sasa wana fursa ya kupinga kuchapishwa kwa taarifa kuwahusu, na wataweza kuzishtaki kampuni zinazofanya hivyo na hata kudai kufidiwa.
Afisa wa serikali anayekiuka maelezo ya sheria hii atatupwa ndani miaka miwili na kulipa faini ya Sh500,000.
Tukizingatia kuwa kampuni nyingi zimekuwa zikihifadhi data kuhusu wafanyakazi wake katika seva na mifumo ya intaneti ya mataifa ya kigeni, sheria hii yafaa kufuatwa.
Wakati wa mgogoro baina ya chama cha ODM na Jubilee hapo 2017 kuhusu matokeo ya kura, suala la ukosefu wa kituo cha kitaifa cha kuhifadhi data liliibuka na ikatakiwa seva za Tume ya Uchaguzi (IEBC) zifunguliwe.
Seva hizo zilikuwa katika taifa moja la kigeni, na kulingana na sheria ya data ya bara Uropa, seva hizo hazingefunguliwa. Unaweza tu kufungua seva iwapo zimewekwa katika taifa unaloishi.
Suala kuu hapa litakuwa iwapo kampuni zitafuata sheria hii, kwa kuwa zimezoa kuvuna hela bila jasho kwa kusambazia mashirika ya kigeni data kuhusu Wakenya.
Ni wakati wa kuwa wazalendo katika biashara zetu, maanake hakuna kampuni ya kigeni itakuja hapa nchini kisha kuuzia kampuni zetu data za siri za mataifa yao.
Kampuni za data za humu nchini sasa zinapaswa kujitahidi kuunda sera za kulinda data za kibinafsi zinazowiana na Sheria ya Data 2019.
Thamani ya data duniani kwa sasa inaipiku ile ya mafuta na gesi, na tunafaa kuilinda kwa mbinu zote kama taifa lenye ushawishi mkubwa zaidi Afrika Mashariki.