• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
NGILA: Data itumike kwa pamoja kufaidi kila mshikadau

NGILA: Data itumike kwa pamoja kufaidi kila mshikadau

Na FAUSTINE NGILA

KATIKA wakati huu wa Mageuzi ya Nne ya Viwanda (4IR), misemo ya kiteknolojia kama ‘data kubwa itavuruga kila sekta’ na ‘data in thamani ya mafuta’ imekuwa ikitumika katika majukwaa mengi.

Hata hivyo, hakuna anayejitokeza kuchambua iwapo misemo hii ni ya kweli hasa katika makuzi ya uvumbuzi na ujasiriamali barani Afrika.

Sipingi kuwa viwanda vingi kwa sasa vinaendeshwa kiteknolojia, ila nalenga kufafanua kuwa mtindo wa data inayotokana na mageuzi ya sasa utakuwa na usemi mkuu kuhusu kampuni itakayotawala sokoni.

Pia kuna mtazamo kuwa wale wanaounda mifumo ya hali ya juu zaidi wataongoza katika umiliki wa masoko ya kidijitali.

Hii inapotosha kwa kuwa tunapoingia 2020, mbinu mpya zinabuniwa kuwafaidi wale wanaofuatilia mageuzi ya kiteknolojia kila siku.

Nimekuwa katika ulingo huu kwa miaka kadhaa sasa, na ningependa kuiambia dunia waziwazi kwamba kigezo cha nani atatawala sokoni kitakuwa kiwango cha muunganisho wa data ainati.

Wale ambao wataunganisha data kutoka wa watu tofauti zaidi wataibuka na usemi mkubwa.

Ili kuwa kiongozi mtajika wa biashara, utahitajika kubuni mifumo ya hali ya juu zaidi na ya aina mbalimbali.

Muunganisho wa data utachochea ubunifu wako, na hapa namaanisha ushirikiano wa mashirika mbalimbali katika matumizi ya data, ili kuongeza kipato.

Mageuzi haya yatazua mabadiliko katika usemi wa kuweka bei, faida na viwango vya mauzo katika mifumo ya sasa ya kibiashara.

Katika karatasi ya kiakademia iliyochapishwa na Kituo cha Maendeleo ya Kimataifa (CGD) kwa kwa jina “Kwaheri kwa Mageuzi Yanayotumia Mifumo ya Kikale”, mwasisi wa kampuni ya mPedigree, Bw Bright Simons anasema kuwa kampuni kubwa za kiteknolojia zinatumia data za wateja bila kujali haki zao.

Kampuni hizi zimezoea kuzoa matrilioni ya faida kutokana na data ya bure, na sasa zinalazimika kukabiliana na athari zinazotokana na mtindo huu.

Tumejionea baadhi ya athari hizi hasa wakati matumizi mabaya ya data kuhusu watu zimechangia kueneza jumbe za chuki na kudidimisha demokrasia duniani.

Nakubaliana na wito wa Bw Simons kwani umechochewa na haja ya kuziba mianya ya ulaghai wa kidijitali kutokana na kasi ya juu ya mauzo kupitia mifumo ya kifedha, na utendakazi wa chini kutokana na hitaji la kampuni hizi la kuongezea mapato.

Hii inafanya vijana wabunifu kufungiwa nje katika makuzi ya kampuni zao ndogo, kwa kuwa hazina data hii. Hivyo, suluhu ni kutumiwa kwa data hii kwa pamoja kufaidi kila mshikadau bila kufungia yeyote nje.

You can share this post!

NGILA: Sharti sote tuheshimu sheria ya kulinda data

INDINDI: Rais atuonyeshe mfano bora katika kuthamini...

adminleo