Moi Dei kuwa Huduma Dei, Boxing Dei kuwa Utamaduni Dei
Na BENSON MATHEKA
Wakenya watakuwa wakitumia tarehe kumi Oktoba kila mwaka kutoa huduma za kujitolea kwa taifa na kwa wasiojiweza katika jamii baada ya Baraza la Mawaziri kubadilisha siku kuu ya Moi Dei kuwa Huduma Dei.
Kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi, baraza la mawaziri pia lilipendekeza sikukuu ya Boxing inayoadhimishwa Desemba 26 kubadilishwa jina kuwa siku ya Utamaduni Dei.
Taarifa kutoka Ikulu ilisema kuwa uamuzi wa kubadilisha sikukuu ya Moi Dei kuwa Huduma Dei, ulitokana na mapenzi ya Rais Mstaafu Daniel Moi, ambaye alitamani kuona ikitumiwa na watu kusaidia wenzao na kujitolea kwa kazi za kitaifa.
Wakenya waliadhimisha siku hiyo kwa mara ya kwanza 1989 kumsherehekea Rais Daniel Moi aliyekuwa akitawala wakati huo.
Katiba mpya ilipopitishwa 2010, haikutambua siku hiyo na aliyekuwa msemaji wa serikali Dkt Alfred Mutua, alitangaza kuwa haingeadhimishwa kwa sababu haikuwa kwenye katiba.
Mnamo 2017, Jaji George Odunga aliamua kwamba ilikuwa sikukuu ya kitaifa na kuagiza kuwa itaendelea kuwa sikukuu ya kitaifa hadi bunge litakapobadilisha sheria ya sikukuu za kitaifa nchini.
Kufuatia uamuzi huo, mwaka 2018 na mwaka huu, waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang’i aliichapisha kuwa sikukuu ya kitaifa katika gazeti rasmi la serikali lakini hakutoa mwongozo kuhusu inavyopaswa kuadhimishwa.
Uamuzi wa baraza la mawaziri wa kubadilisha jina la siku kuu hiyo kuwa Huduma Dei sasa utatoa mwongozo wa jinsi Wakenya watakuwa wakiisherehekea. Aidha, utakomesha mjadala kuhusu iwapo siku hiyo inapaswa kuendelea kuwepo au la.
Mwaka jana, msemaji wa Rais Mstaafu Moi alisema rais huyo wa pili wa Kenya Lee Njiru angetaka siku hiyo itumiwe kusaidia masikini katika jamii.
Baraza la mawaziri lilisema kuwa siku ya Utamaduni Dei itakuwa ikitumiwa kusherehekea utamaduni mpana wa Wakenya.
Hata hivyo, sikukuu hizo mbili zitaanza kuadhimishwa mabadiliko hayo yakipitishwa na bunge.Katika ripoti ya Jopokazi la Maridhiano iliyotolewa mwezi jana ilipendekezwa kuwa Desemba 26 ibadilishwe kuwa siku ya Wakenya kusherehekea utamaduni wao.
Kamati iliyotayarisha ripoti hiyo ilisema siku hiyo inayoadhimishwa baada ya Krisimasi inafaa kuitwa National Culture Day.