• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Uhuru, Raila na Ruto wamng’ang’ania Mudavadi

Uhuru, Raila na Ruto wamng’ang’ania Mudavadi

Na OSCAR OBONYO

KIONGOZI wa Chama cha Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi, ameanza kumezewa mate na mirengo tofauti ya kisiasa nchini, kila upande ukitaka kuungana naye kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Wanaomwinda ni Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga huku siasa zinazoendelea za kumrithi Rais Uhuru Kenyatta zikishika kasi.

Rais Kenyatta naye ameonekana kujiingiza katika mg’ang’anio huo kwa kujaribu kumleta karibu Bw Mudavadi.

Akizungumzia wanasiasa ambao wanajaribu kumrai aungane nao, kiongozi huyo wa ANC anasema hivi: “Watu wanajitetea kwa umbali baada ya kugundua kuwa Musalia ndiye mpishi ambaye Wakenya wanataka.”

Mwaliko ambao Rais Kenyatta alimpa Mudavadi wakasafiri kwa helikopta yake (Rais) hadi Garissa imewaacha wengi na maswali kuhusu ikiwa wawili hao wanapanga kubuni muungano wa kisiasa au la.

“Nilikuwa Garissa kwa mwaliko wa Rais. Kwa hivyo, ni yeye anafahamu ni kwa nini mimi ndiye alinialika kwa safari hiyo wala sio mwingine. Kwa hivyo, wale ambao wanataka kuingiza siasa katika safari hiyo wako huru kufanya hivyo,” Bw Mudavadi aliambia Taifa Jumapili, alipoulizwa kuhusu safari hiyo.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa ANC hakukanusha madai kuwa yeye na Rais Kenyatta wamekuwa karibu.

“Mimi na Rais tumekuwa marafiki kwa muda mrefu. Ikiwa urafiki huo unaweza kuchangia kuboresha usimamizi wa taifa letu kwa manufaa ya Wakenya wote, sina shida,” alisema.

Rais Kenyatta na Mudavadi, ambao walizaliwa mnamo 1960 walifundishwa siasa na Rais mstaafu Daniel Moi.

Aliwateua wawili hao kuwa mawaziri katika serikali yake na warithi wake mnamo 2002- Kenyatta akiwa mgombeaji urais na Mudavadi akitengewa wadhifa wa Makamu wa Rais.

Ingawa yeye pia anaandaa kampeni zake za urais kuelelekea uchaguzi mkuu wa 2022, wanasiasa wandani wa Dkt Ruto na Bw Odinga wamekuwa wakijaribu kumleta karibu makamu huyo wa rais wa zamani.

Seneta wa zamani wa Kakamega Bonny Khalwale ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto ameungama kuwa yeye ni mmoja wa wanasiasa kutoka Magharibi mwa Kenya ambao wanaendeleza mazungumzo “ili Ruto na Mudavadi wafanyekazi pamoja kuelekea 2022.”

Hata baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu wa 2022, Kenyatta na Mudavadi walidumisha uhusiano wa karibu pale Bw Kenyatta alipomwalika Mudavadi kuwa mgombea urais katika muungano wa kisiasa waliobuni na William Ruto mnamo 2012.

Wakati huo, Kenyatta na Ruto walikuwa wakikabiliwa na kesi katika Mahama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na ndipo wakaamua kumuunga mkono Mudavadi kama mgombea urais.

Lakini mpango huo ulisambaratika Kenyatta na Ruto walipobadili nia kutokana na kile Rais alidai, wakati ni “kupotoshwa na pepo”.

Lakini wakati huu uhusiano kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto sio mzuri huku kukitokea minong’ono kwamba kiongozi wa taifa na Bw Odinga huenda wakampendekeza tena Bw Mudavadi kuwa mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Na licha ya tofauti “kidogo” zilizoibuka kati ya kiongozi huyo wa ANC na Bw Odinga kuhusu yaliyomo kwenye wasifu wake “Storm of Passion” anashikilia kuwa angali rafiki wa kiongozi huyo wa ODM.

“Ikiwa kuna tofauti zozote kati yangu na yeye, basi hizo ni fikra za wale ambao wanatoa madai hayo;” Bw Mudavadi akasema.

Naye naibu kiongozi wa ANC Ayub Savula anamtaka Bw Mudavadi kufanyakazi na Rais Kenyatta pamoja na Bw Odinga.

“Wakati huu ambapo uhusiano kati ya Rais na Naibu wake sio mzuri, namshauri kiongozi wetu kufanyakazi na Rais na Bw Odinga,” akasema Mbunge huyo wa Lugari.

You can share this post!

Hatari ya kujianika mitandaoni msimu huu wa Krismasi

Mutula Kilonzo ajitetea kumwakilisha Sonko

adminleo