• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 2:08 PM
JAMVI: Mutua alitishwa na Ruto au ni siasa tu?

JAMVI: Mutua alitishwa na Ruto au ni siasa tu?

Na BENSON MATHEKA

Madai ya Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua kwamba alitishiwa maisha na Naibu Rais William Ruto na washirika wake Aden Duale (kiongozi wa wengi katika bunge) na Kipchumba Murkomen (kiongozi wa wengi katika seneti) yanalenga kutimiza maslahi ya kisiasa, japo hayafai kupuuzwa, wadadisi wanasema.

Ingawa ni jukumu la polisi kuchukua hatua kubainisha ukweli wa madai hayo, wadadisi wanasema akiwa mwanasiasa aliye na azima ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 ambao Dkt Ruto anamezea mate, huenda Dkt Mutua alilenga kujijenga kisiasa.

Na kuna wanaohisi kuwa ikizingatiwa kwamba Gavana Mutua anataka kutambuliwa kama msemaji wa jamii ya Wakamba, madai yake dhidi ya Naibu Rais yanaweza kuwa sehemu ya njama pana ya kuonyesha anaungwa mkono na watu wengi kutoka ngome yake.

“Kuna kila dalili kwamba madai hayo ni mpango mkubwa wa kutimiza malengo ya kisiasa na Dkt Mutua alitekeleza sehemu ya mpango wenyewe. Akiwa mtaalamu wa mawasiliano, Dkt Mutua anajua umuhimu wa kutumia kila tukio kuwasilisha ujumbe fulani na kutimiza malengo fulani,” asema mdadisi wa siasa James Kisilu.

Ikizingatiwa kwamba madai hayo yalijiri wakati ambao mpinzani wake mkuu eneo la Ukambani, kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka anadaiwa kuwa na mipango ya kushirikiana na Dkt Ruto kuelekea 2022, madai hayo hayakosi chembe za siasa.

Bw Musyoka amekanusha madai ya aliyekuwa seneta wa Machakos Johnstone Muthama kwamba anapanga kuungana na Dkt Ruto.

“Siku moja baada ya Dkt Mutua kuandikisha taarifa yake kwa polisi, watu walijitokeza kwenye barabara za miji mikuu katika kaunti tatu za Ukambani kuandamana wakikashifu Dkt Ruto, Duale na Murkomen. Hii ilipangwa ili kuonyesha kuwa gavana huyo ni maarufu kote Ukambani,” alisema Bw Kisilu.

Dkt Mutua alisema kuwa Bw Duale na Bw Murkomen walikuwa wa kwanza kumtishia maisha, walipokutana Ikulu alikoalikwa Rais alipopokea ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI).

Gavana huyo anadai kwamba wawili hao walimlaumu kwa kumshambulia Dkt Ruto na kuapa kumfunza adabu.

Anaeleza kuwa alikutana na Naibu Rais Ikulu Desemba 11, ambapo alitisha kumwangamiza kwa kuendelea kumshambulia.

Ingawa wadadisi wanasema kuwa ni vigumu kuamini na kuchunguza madai hayo ikizingatiwa hadhi ya wanaolaumiwa na mahali vitisho vinadaiwa kutolewa, Dkt Mutua anasisitiza kuwa nchi hii ina historia ya mauaji na anahisi maisha yake yamo hatarini.

“Madai hayo hayawezi kuchunguzwa bila kuandikisha taarifa kutoka kwa wanaolaumiwa na walioshuhudia. Ikizingatiwa anaotaja kwenye taarifa yake ni wanasiasa wakiwemo wanaoweza kuwa mashahidi, inaweza kuwa vigumu kuendelea na kesi hii isipokuwa kwa na shinikizo kutoka kwa watu wenye ushawishi,” aeleza Bw Victor Wambi, mtaalamu wa masuala ya upelelezi na usalama.

Kulingana na Dkt Mutua, alikuwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga Ikulu siku anayodai Dkt Ruto alimtishia maisha.

Katika taarifa yake kwa polisi, gavana huyo anasema alipomsalimu Dkt Ruto, alimfinya mkono kwa nguvu na akiwa na hasira kali akamuonya: “Umekua ukinichapa sana na lazima sasa nikugonge…Nitakugonga.”

Alisema aliamua kuripoti kwa polisi baada ya kushauriana na maafisa wakuu wa serikali, viongozi wa kisiasa na familia yake.

“Hii inafanya watu kuhisi kuwa hatua ya Dkt Mutua ni ya kisiasa ikizingatiwa kuwa ameegemea sana upande wa Bw Odinga katika kile kinachoonekana kumtenga Bw Musyoka na waziri huyo mkuu wa zamani. Isisahaulike kwamba Dkt Ruto na Bw Odinga ni mahasimu wa kisiasa,” asema Bw Kisilu.

Kulingana na washirika wa Dkt Ruto akiwemo Murkomen na Duale, madai ya Gavana Mutua ni ya kubuni ili kutafuta umaarufu.

“Hauwezi kupata umaarufu kwa kutaja majina ya viongozi ambao wameafikia mengi kuliko unayoweza kutimiza,” Bw Duale alimweleza Dkt Mutua.

Lakini Bw Wambi anasema madai ya vitisho dhidi ya kiongozi au mtu yeyote hayafai kupuuzwa. “ Uchunguzi unafaa kufanywa ili kubaini ikiwa Gavana Mutua alibuni vitisho hivyo au la,” aeleza.

Anasema kwa vile Dkt Mutua alisema alikuwa na Bw Odinga alipotishiwa maisha na Dkt Ruto, kiongozi huyo wa ODM anachukuliwa kuwa shahidi iwapo polisi wataamua kuchunguza madai hayo.

Kulingana na Dkt Mutua, vitisho dhidi yake vinatokana na msimamo wake kuhusu vita dhidi ya ufisadi na kauli zake kuhusu Ruto na washirika wake wa kisiasa.

“Nimekuwa nikiunga pendekezo watumishi wa umma wakaguliwe mitindo yao ya kimaisha na maafisa wafisadi waondoke mamlakani na ninadhani niliwakasirisha,” asema.

Wandani wa Dkt Ruto, akiwemo Murkomen walipinga pendekezo hilo wakisema lililenga Dkt Ruto.

Wakenya wanasubiri kuona polisi watakavyoshughulikia ripoti ya Dkt Mutua na joto la kisiasa ambayo huenda ikazua siku zijazo.

You can share this post!

DINI: Uwe baraka kwa wengine msimu huu jinsi Mungu...

JAMVI: Uhuru anatatiza shughuli za IEBC na mahakama...

adminleo