JAMVI: Uhuru anatatiza shughuli za IEBC na mahakama kimakusudi
Na LEONARD ONYANGO
HATUA ya Idara Korti ya Rufaa kusitisha shughuli zake katika maeneo yote ya nchi isipokuwa Nairobi kutokana na uhaba wa majaji, imeibua mjadala kuhusu haja ya kufanyia katiba mabadiliko ili kumpokonya rais baadhi ya mamlaka.
Kiongozi wa Mahakama ya Rufaa William Ouko Ijumaa alisema kuwa korti hiyo itafunga korti zake zilizoko katika Kaunti za Kisumu, Nyeri na Mombasa kuanzia Januari 13.
Jaji Ouko alisema kuwa mahakama ya rufaa imesalia na majaji 15 na wawili kati yao hawasikizi kesi kwani wanatekeleza majukumu mengine.
Uhaba wa majaji wa Mahakama ya Rufaa umesababishwa na hatua ya Rais Kenyatta kukataa kuteua rasmi majaji 41 waliofaulu katika mahojiano yaliyoendeshwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).
Majaji 41 hao wanajumuisha wale wa mahakama ya Rufaa, Ardhi na kushughulikia masuala ya Ajira.
JSC iliteua majaji 11 kwa ajili ya Mahakama ya Rufaa ambao ni Francis Tuiyot, Weldon Korir, Mbogholi Msagha, Aggrey Muchelule, George Odunga, Joel Ngugi, Hellen Omondi, Pauline Nyamweya, Jessie Lesiit, Mumbi Ngugi na Kibaya Laibuta.
JSC ilipowasilisha majina ya majaji hayo, Rais Kenyatta hakuyachapisha katika Gazeti Rasmi la Serikali akidai kuwa baadhi ya majaji walioteuliwa na JSC walikuwa na dosari za kimaadili.
Baadhi ya mawakili wameenda katika Mahakama Kuu kumshinikiza Rais Kenyatta kuchapisha majina hayo kwenye Gazeti Rasmi la Serikali.
Lakini Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua alipofika kortini kwa niaba ya rais, alisema kuwa baadhi ya majaji hao wana dosari.
Alishangaa ni kwa nini JSC ilipuuza malalamishi yaliyowasilishwa dhidi ya baadhi ya majaji hao.
“Rais alipokea ripoti zilizofichua kuwa baadhi ya majaji walioteuliwa wana matatizo ya kimaadili,” akasema Bw Kinyua.
Aliyekuwa Rais wa chama cha Wanasheria Afrika Mashariki James Mwamu anasema kuwa Rais Kenyatta anafaa kuchapisha majina ya majaji hao na kisha apendekeze kubuniwa kwa jopo la kuwachunguza wale anaohisi kwamba wana dosari.
“Kabla ya JSC kuteua majaji inapokea ripoti kutoka kwa idara mbalimbali, ikiwemo Idara ya Ujasusi (NIS). Mbona NIS hawakufahamisha JSC na wakampelekea ripoti rais?,” anahoji Bw Mwamu.
Anasema kuwa Rais Kenyatta ana wawakilishi wanne, akiwemo Mkuu wa Sheria, ambao walifaa kuhakikisha kuwa malalamishi yaliyowasilishwa dhidi ya baadhi ya majaji yanazingatiwa kabla ya kufanya uteuzi.
Wakili Otiende Amollo anasema si jukumu la rais kufanya uchunguzi kuhusu majaji kwani kazi yake ni kuchapisha majina yao kwenye Gazeti Rasmi la Serikali.
Wakili Ahmednasir Abdullahi anasema kuwa matatizo yanayokumba Idara ya Mahakama yanasababishwa na tume ya JSC.
“Serikali ya Jubilee imefanikiwa kuteka nyara JSC na hakuna anayezungumza kwa niaba ya Idara ya Mahakama,” anasema Abdullahi.
Rais Kenyatta pia ameshutumiwa kwa kulemaza shughuli za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) baada ya kukataa kuchapisha kwenye gazeti rasmi nafasi zilizoachwa wazi na makamishna waliojiuzulu.
Naibu mwenyekiti wa IEBC Connie Nkatha Maina pamoja na makamishna Margaret Mwachanya na Paul Kurgat walijiuzulu mnamo Aprili 2018 wakidai kuwa mwenyekiti wao Wafula Chebukati alishindwa kuonyesha uongozi ufaao.
Kamishna Roselyne Akombe alijiuzulu kabla ya uchaguzi wa urais wa marudio Oktoba 26, 2017.
Tume ya IEBC sasa imesalia na makamishna watatu: Mwenyekiti Wafula Chebukati, Abdi Guliye na Boya Molu.
Kimya cha Rais Kenyatta kuhusiana na makamishna hao waliojiuzulu umesababisha wabunge kuanza mchakato wa kubadilisha sheria ili kuhakikisha kuwa nafasi katika tume ya IEBC zinajazwa hata bila rais kuzitangaza katika Gazeti Rasmi la Serikali.
Bw Chebukati pia anaunga mkono pendekezo hilo la wabunge.
Mswada unaotoa mwongozo kuhusu namna ya kujaza nafasi zinazoachwa wazi na makamishna wa IEBC tayari umepitishwa na Bunge la Kitaifa.
Mswada huo sasa uko mbele ya Bunge la Seneti na umeidhinishwa na Kamati ya Seneti kuhusu masuala ya Sheria.