Miamba wa soka duniani
NA MASHIRIKA
DOHA, QATAR
KOCHA Jurgen Klopp alikuwa mwingi wa sifa kwa masogora wake wa Liverpool kwa “kupita mtihani mwingine” baada ya miamba hao wa soka ya Uingereza na bara Ulaya kutandika kikosi cha Flamengo na kunyanyua ubingwa wa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.
Nyota Roberto Firmino aliwafungia Liverpool bao la pekee na la ushindi katika muda wa ziada na kuwapa waajiri wake ushindi wa 1-0 dhidi ya miamba hao wa soka ya Brazil ugani Khalifa, Qatar.
Kombe hilo lilikuwa la pili kwa Liverpool kutia kibindoni msimu huu baada ya kuwachabanga Chelsea mnamo Agosti na kutawazwa mabingwa wa Uefa Super Cup.
“Vijana walijituma ipasavyo na kusajili matokeo ya kuridhisha. Maisha yao yamekuwa ya mtihani baada ya mwingine. Tija zaidi ni kwamba wamekuwa wakiibuka washindi mwishoni mwa kila mjarabu,” akasema Klopp.
Awali, Monterrey kutoka Mexico walikuwa wamewapepeta Al Hilal ya Saudi Arabia 4-3 kupitia penalti na kumaliza kampeni za Kombe la Dunia katika nafasi ya tatu. Mshindi wa mchuano huo aliamuliwa kupitia penalti baada ya vikosi vyote viwili kuambulia sare ya 2-2 mwishoni mwa muda wa ziada.
Ni matarajio ya Klopp kwamba ushindi wa Liverpool utawatambisha hata zaidi katika michuano ijayo kadri wanavyojiandaa kwa ratiba ngumu ya Krismasi na Mwaka Mpya.
Ratiba ya kivumbi cha Kombe la Dunia iligongana na kipute cha Carabao Cup ambacho Liverpool walikuwa pia wakiwania msimu huu.
Hivyo, ilimweka Klopp katika ulazima wa kutuma kikosi kingine cha chipukizi wa Liverpool uwanjani Villa Park kuchuana na Aston Villa katika nusu-fainali ya Carabao. Hata hivyo, makinda hao wa Liverpool walipokezwa kichapo cha 5-0.
Liverpool kwa sasa wanajiandaa kushuka dimbani kumenyana na Leicester City katika mchuano wa EPL ambao umeratibiwa kuwakutanisha Alhamisi hii uwanjani King Power. Wataingia katika mechi hiyo wakijivunia pengo la alama 10 kileleni mwa jedwali la EPL.
Ushindi wa 3-1 uliosajiliwa na Manchester City dhidi ya Leicester ugani Etihad mnamo Jumamosi ulipunguza pengo la pointi kati ya washindani hao wakuu hadi alama moja pekee. Leicester kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili jedwalini kwa alama 39 kutokana na mechi 18 zilizopita.
“Nimejitahidi sana kutafuta maneno ya kuelezea heshima yangu kwa vijana hawa wa Liverpool. Wamekuwa wakifanya mambo mazuri na ya kutia moyo zaidi katika takriban kila pambano,” akasema Klopp.
Pigo la pekee kwa Liverpool kwa sasa ni jeraha ambalo linatarajiwa kumweka kiungo Alex Oxlade-Chamberlain mkekani kwa kipindi kirefu kijacho.
Mwingereza huyo mwenye umri wa miaka 26 alionekana akitembelea mikongojo Liverpool walipokuwa wakisherehekea ushindi mwishoni mwa mechi. Oxlade-Chamberlain aliondolewa uwanjani mapema katika kipindi cha kwanza baada ya kuanguka vibaya na kuumia.
Firmino ndiye aliyewafungia Liverpool bao la ushindi dhidi ya Monterrey katika hatua ya nusu-fainali ya Kombe la Dunia. Liverpool ndicho kikosi cha pili kutoka Uingereza baada ya Manchester United mnamo 2008 kutia kapuni ubingwa wa Kombe la Dunia.