• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 11:34 AM
Kalonzo aomba msamaha kuungana na Uhuru

Kalonzo aomba msamaha kuungana na Uhuru

Na BONIFACE MWANIKI

KIONGOZI wa Chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka ameomba msamaha viongozi waasi wa eneo la Ukambani, na kuwataka waungane naye ili kutafuta Urais ifikapo mwaka wa 2022.

Akizungumza na viongozi mbalimbali kutoka eneo la Ukambani wakati wa kongamano kubwa katika makazi yake katika eneo la Yatta, Bw Musyoka alisema wakati umefika kwa eneo hilo kuzungumza kwa sauti moja.

Makamu huyo wa rais wa zamani alisema kama aliwakosea viongozi kutoka eneo hilo, wamsamehe kwa hatua yake ya kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta.

“Ningependa kuwaomba msamaha viongozi wote ambao hawakufurahia hatua yangu ya kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta wakati tulipokuwa kwenye mazishi ya marehemu babangu,” aliongeza.

Alisema amani ni muhimu nchini kwa hivyo viongozi waunge mkono juhudi za Rais Kenyatta kuleta umoja wa taifa.

Hata hivyo, magavana wote watatu wa eneo la Ukambani ambao wamekuwa wakionekana kujitenga na Bw Musyoka hawakuhudhuria mkutano huu. Wao ni Bi Charity Ngilu (Kitui), Prof Kivutha Kibwana (Makueni) na Dkt Alfred Mutua (Machakos)

Kiongozi huyo wa Wiper alidai aliwapigia simu, na wote wakatoa ahadi kuwa wangefika au kutuma wawakilishi.

Bw Musyoka alisema hana uhasama wowote na kiongozi yeyote kutoka eneo la Ukambani na yuko tayari kufanya kazi na viongozi wote bila ubaguzi.

Aliitaka jamii ya Wakamba kuunga mkono ripoti ya Jopokazi la Maridhiano almaarufu (BBI).

“Amani ni muhimu sana na ningependa Viongozi wote kutoka eneo hili waungane,” aliongeza.

Hata hivyo, Bw Musyoka alitaka nafasi ya waziri mkuu kuongezwa nguvu zaidi, ili kumpa uwezo wa kutenda kazi vizuri na kupunguza nguvu za Rais.

“Kwa jumla naunga mkono hii ripoti ya BBI, lakini nina tashwishi kuhusu mamlaka aliyopewa waziri mkuu kwenye ripoti hii. Tungependa mamlaka yake yaongezwe na achaguliwe na wabunge wala si Rais kama ilivyopendekezwa, ili aweze kutenda kazi vyema na kumdhibiti rais atakayechaguliwa,” alisisitiza Bw Musyoka.

You can share this post!

Madiwani 18 wala njama ya kumwokoa Sonko

Msongamano Krismasi: KeNHA yatangaza barabara mbadala

adminleo