• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
2019 ulikuwa mwaka wa mauaji ya kifamilia

2019 ulikuwa mwaka wa mauaji ya kifamilia

Na MARY WANGARI

MWAKA huu ulikumbwa na visa tele vya mauaji ya kifamilia hasa yaliyosababishwa na tofauti za kindoa.

Visa hivi vilihusu pia wapenzi waliotemwa wakilipiza kisasi kwa kuwaua wenzao au mume na mke wakigeukiana na kuuana.

Wakenya wangali wametikiswa na kisa ambapo mwanajeshi wa KDF ameshtakiwa kwa mauaji ya mkewe na watoto wao wawili waliopatikana wamezikwa katika kaburi moja mnamo Novemba.

Meja Peter Mugure, 34, alidaiwa kumuua mkewe Joyce Syombua na watoto wao Shanice Maua, 10, na Prince Michael, 5 na kisha kuwazika pamoja eneo la Thingithu.

Mnamo Oktoba, simanzi ilitanda kufuatia ripoti kuhusu mwanamume Charles Muriuki, 45, aliyedaiwa kumuua mtoto wa mpenziwe kufuatia mafarakano kati yao.

Bw Muriuki alishtakiwa kwa mauaji ya mtoto huyo mwenye umri wa miaka 11 katika eneobunge la Mathira, Kaunti ya Nyeri na kisha kuuzika mwili wake katika Msitu wa Ragati.

Lakini pana kisa kilichoshangaza hata zaidi; mwanamke mwenye umri wa miaka 26 alifariki baada ya kumiminiwa petroli na kuunguzwa kwa moto na mumewe nyumbani kwao, Nakuru, Mama huyo wa watoto wawili alikata roho baadaye hospitalini alipokuwa akitibiwa baada ya kuchomeka asilimia 25.

Mauaji ya kinyama ya Emma Wanyotta, mwanafunzi wa Chuo cha Urembo cha Vera mjini Eldoret ni kisa kingine cha Oktoba kilichowasikitisha wengi.

Mwili wa marehemu ulipatikana katika shamba lililokuwa karibu na kwao ambapo mpenziwe, aliyetajwa kama jambazi sugu, alihusishwa na mauaji hayo.

Mnamo Agosti, wakazi katika kijiji cha Mirangine, Kaunti ya Nyandarua, walibaki vinywa wazi baada ya mwanamume mwenye umri wa miaka 30 kuwaua kikatili wanawe wawili kwa kuwadunga kisu na kisha kujitia kitanzi. Katika kisa cha kushangaza hata zaidi mnamo Agosti vilevile, mwanamume aliwaua kwa kuwakatakata watoto wake wenye umri wa miaka sita na miaka minne Kaunti ya Bomet, baada ya kugombana na mkewe kuhusu unga wa mahindi.

Peter Langat aliyekuwa mfanyakazi katika kiwanda cha chai cha Shiomo, alitoweka baada ya kutekeleza unyama huo huku mkewe, mwalimu wa ECD, akiponea chupuchupu tukio hilo la kutisha.

Mnamo Julai, taifa lilitikiswa na habari kuhusu mwanamke mwenye umri wa miaka 32 aliyemvamia mumewe kwa shoka na kumuua na kisha kuwanyonga watoto wake wawili wa umri wa miaka 14, na 3, kabla ya kujitia kitanzi nyumbani kwao eneo la Thome, Nairobi.

Mnamo Mei, Wakenya waliamkia habari za kushtusha kuhusu mauaji ya afisa wa polisi Konstebo Pauline Wangari. Mlinzi huyo wa gereza aliuawa kwa kudungwa kisu eneo la Murang’a na mpenziwe Joseph Ochieng, walliyekutana kupitia mitandao ya kijamii

Mwezi huo huo, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Methodist (KEMU) Ann Kanario, 21, alipatikana akiwa amefariki chumbani mwake chuoni humo.

Polisi walishuku kuwa marehemu aliuawa na mpenziwe Obed Nyaga Njahi, ambaye mwili wake pia ulipatikana ukining’inia chumbani humo.

Katika kisa kingine kilichotikisa nchi na mataifa ni kuhusu mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Moi Ivy Wangechi, aliyeuawa kwa kukatwa na shoka mchana mnamo Aprili.

Mpenziwe Naftali Kinuthia, baadaye alikiri kutekeleza unyama huo akidai marehemu alikuwa hampendi hakumrejeshea mapenzi.

You can share this post!

Mutua sasa atishia kumwaga mtama kuhusu ghasia za 2007

2019: Sarakasi bungeni hazikukosa hata Akothee na minisketi...

adminleo