• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Maendeleo yalivyokwama Zimmerman kutokana na mzozo wa ardhi

Maendeleo yalivyokwama Zimmerman kutokana na mzozo wa ardhi

NA SAMMY WAWERU

Ujenzi wa soko la Zimmerman Settlement Scheme, pembezoni mwa Thika Super Highway eneo la Carwash lililoko mtaa wa Zimmerman kaunti ya Nairobi ulianza kwa kishindo mnamo 2014.

Bi Elizabeth Mwangi ni mmoja wa waliovutiwa na mradi huo wa maendeleo na bila kupoteza wakati akawekeza humo kwa kununua vipande viwili vya ardhi, kila kimoja akiuziwa Sh250, 000.

“Kimoja kina ukubwa wa mita 10 kwa 10, mraba. Nilikuwa nimeanza kujenga ili niwe miongoni mwa watakaofungua soko hilo,” Bi Mwangi anaiambia Taifa Leo Dijitali.

Kilichomtia motisha ni kasi iliyowekwa wakati wa ujenzi, na matumaini waliyokuwa nayo wawekezaji kupitia ushawishi wa chama cha ushirika cha Zimmerman Settlement Scheme.

Hata hivyo, soko hilo sasa ni mahame baada ubomoaji uliofanywa mwaka huu kwa kinachodaiwa kuwa mzozo wa ardhi.

“Nilikadiria hasara ya maelfu ya pesa. Nina ithibati ya umiliki wa ardhi nilizonunua na nina matumaini mambo yakitatuliwa tutarejea kukuza eneo hilo,” anasema mama huyo, akiongeza kusema kwamba fedha alizotumia zilikuwa baadhi ya pensheni yake.

Zimmerman Settlement Scheme inakadiriwa kuwa na zaidi ya ekari 200, na ambazo maelfu ya watu wamewekeza kwa ujenzi. Ukiwa katika barabara ya Thika Super Highway, utatazama majumba mengi ya kupangisha na mengine ya kifahari ya kibinafsi.

Hata ingawa eneo hilo lina historia yake, linaonekana kukua kwa mwendo wa kasi. Kwa wanaolielewa kwa kina, wanasema kabla ya 2016, eneo hilo lilikuwa limesheheni vichaka na fichio na hifadhi la wahuni waliotekeleza uhalifu Thika Super Highway.

“Awali wahalifu katika mitaa jirani ya Githurai na Kasarani walikuwa wakijificha humu. Sasa si mafichio tena ila makazi ya maelfu ya watu,” aeleza Peter Kioko mkazi.

Chini ya aliyekuwa gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero, Carwash Zimmerman ilishuhudia mabadiliko makuu kimaendeleo.

Dkt Kidero alishirikiana sako kwa bako na wasimamizi wa Zimmerman Settlement Scheme ili kuona waliowekeza humo wamefanikisha maendeleo.

Licha ya ubomozi wa baadhi majengo, shule kadha za msingi japo za kibinafsi zimejengwa, kama vile Penda Elimu School na Kisima School. Eneo hilo pia lina kituo kimoja cha afya.

Isitoshe, hali ya usalama imeimarishwa kwa kuwepo kwa kituo cha askari, Kenya Police Service Zimmerman.

Miundo msingi kama vile barabara na mataa ya miji maarufu kama street lighting kwa Kiingereza, inaendelea kuimarishwa.

“Kinachotushangaza ni kuona majengo yakibomolewa ilhali baadhi ya huduma kama usambazaji wa nguvu za umeme, maji na mitaro ya majitaka, zote ziliidhinishwa na serikali kupitia asasi husika,” alalamika Irene Wanjiku, mmoja wa wamiliki.

Kimsingi, eneo hilo limekua kwa ushahidi wa biashara zilizonoga na kunawiri. Licha ya hilo, baadhi ya wamiliki wameonekana kuwa na kiwewe na wasiwasi kuendeleza ujenzi, kwa mujibu wa majengo yaliyositishwa kujengwa, (tazama pichani).

Francis Kirima, mwenyekiti wa Zimmerman Settlement Scheme anaishangaa serikali ya Jubilee ikipigia upatu ujenzi wa nyumba bora na za bei nafuu, ilhali zilizoko inaendelea kuzibomoa.

“Huu ni mradi wa maskwota na ardhi tunayoendelea kujenga tuliipata kwa njia halali. Si ya kunyakua wala eneo la chemichemi. Tunaomba Rais wetu tuliyemchagua Uhuru Kenyatta atuunge mkono tuafikie ajenda ya ujenzi wa nyumba,” afafanua Bw Kirima.

Ujenzi wa nyumba bora na za bei nafuu ni mojawapo ya nguzo nne kuu, alizozindua Rais Kenyatta ipatayo miaka miwili iliyopita. Ufisadi umegubika serikali ya Jubilee, idara ya ardhi ikiwa mojawapo ya zisizokosa kuhusishwa na sakata.

Bw Kirima anahisi huenda kuna mchezo unaosakatwa chini kwa chini na baadhi ya mabwanyenye serikalini, kufurusha anaotaja kama maskwota wanaomiliki eneo hilo.

Wakati wa ubomoaji, gavana wa Nairobi Mike Sonko na ambaye kwa sasa anaandamwa na masaibu ya ufisadi, ubadhirifu wa fedha miongoni mwa tuhuma zingine, alizuru vifuzi vya soko la Zimmerman Settlement Scheme akahakikishia wamiliki kuwa ardhi yao haitanyakuliwa.

Kwa kile kilionekana kama kufariji wamiliki waliojawa na ghadhabu wakati huohuo nyoyo zao zikidunda kwa kubomolewa majengo na hofu shughuli hiyo itaendelea, Bw Sonko alisema amewasiliana na Rais Kenyatta aliyeamuru ubomoaji usitishwe mara moja.

“Nikifanya kampeni kuomba kura mnichague, niliahidi kutetea wanyonge wasidhulumiwe. Hakuna ubomoaji utakaofanyika tena, na ni suala ambalo limelifikisha kwa Rais,” alisema gavana huyo.

Carwash Zimmerman ni eneo ambalo likijengwa kikamilifu, litasiri maelfu ya watu, ikizingatiwa kuwa ada ya nyumba ni nafuu. Isitoshe, litabuni maelfu ya kazi hususan kwa wanaopania kuwekeza kwenye biashara.

Shughuli za usafiri na uchukuzi, si kikwazo kwani Thika Super Highway, ambayo ni barabara kuu nchini i mkabala. Inachopaswa kufanya serikali ni kuangazia mzozo wa ardhi ya mradi huo, iutatue, ili kutuliza nyoyo za wawekezaji waendelee kujenga taifa.

 

You can share this post!

KRISMASI: Hofu wasichana wakijikeketa wenyewe

SYOKAU NZOMO: Namshukuru Mola nang’aa kwa usanii wa...

adminleo