• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
AKILIMALI: Mchana mkulima, jioni mwanabodaboda

AKILIMALI: Mchana mkulima, jioni mwanabodaboda

NA SAMMY WAWERU

Ukizuru eneo la Ngoingwa, Thika utalakiwa na mandhari ya hadhi ya juu kutokana na majumba ya kifahari yaliyojengwa.

Hata ingawa mengi ni ya kibinafsi, kuna kadha ya kupangisha ili kusitiri wenye mapato ya kadri na yale madogo. Ni katika eneo lilo hilo barabara kuu inayoungisha mji wa Thika na Naivasha na Limuru imepitia.

Licha ya sifa hizo za kipekee, Ngoigwa ambayo inapatikana katika kaunti ya Kiambu, ina mashamba yanayoendeleza shughuli za kilimo. Hii ina maana kuwa mabwanyenye na wakazi kwa jumla, hawahangaiki kupata mazao ya kilimo. Isitoshe, wanapata mazao yanayotoka moja kwa moja shambani.

Katika mojawapo ya mgunda tunapatana na kijana Eric Mutunga, anayekuza mseto wa mboga. Aidha, huzalisha sukuma wiki, spinachi, mboga za kienyeji kama vile mnavu almaarufu sucha au managu, ikiwa ni pamoja na mchicha (terere).

Bw Mutunga, 27, pia hukuza broccoli – mboga nadra kupatikana na yenye manufaa chungu nzima kisiha, pilipili mboga (wengi wanaifahamu kama hoho) na vilevile nyanya.

Barobaro huyo anayetoka Masaku, Kaunti ya Machakos anasema alihamia eneo la Thika miaka kadha iliyopita, ili kusukuma gurudumu la maisha. Kabla kuingilia shughuli za kilimo, gange iliyomkaribisha ni ya ukeateka wa jumba la kupangisha la bwanyenye mmoja eneo hilo.

Kwa kuwa ni kazi yenye muda mwingi wa ziada kupumzika hasa baada ya shughuli za usafi majira ya asubuhi, Mutunga anasema aliwaza na kuwazua jambo analoweza kufanya ili kupiga jeki mapato yake. Kulingana na simulizi yake, wazo lililomjia ni kununua punda na kijigari chake (mkokoteni), na punde si punde akaanza kubebea watu mizigo.

“Wateja wengi walikuwa wakulima na kina mama wa sokoni niliowasafirishia mazao kutoka shambani hadi sokoni,” adokeza kijana huyo. Uchukuzi kwa njia ya punda pia ulijumuisha wenye maduka na mikahawa, kubebewa bidhaa.

Hata hivyo, mwaka uliopita, jitihada zake nusra zizimwe alipohusika katika ajali mbaya na punda wake. “Nilivunjika mguu baada ya kuangushwa na punda nikiwa kwenye mkokoteni,” anasimulia.

Maisha lazima yangesonga mbele, familia yake; mkewe na mtoto mmoja wapate riziki, na kwa kuwa alikuwa ametangamana na wakulima wengi alishawishika kuingilia kilimo, alipopata nafuu.

Miaka miwili baadaye, Mutunga hajutii kamwe, badala yake ana kila sababu ya kutabasamu. Mtaji wa takriban Sh20, 000 aliowekeza katika ukuzaji wa mimea mseto, sasa unamuingizia mapato yasiyopungua Sh1, 500 kila siku, akiondoa gharama ya matumizi.

Aidha, gharama ni ununuzi wa pembejeo kama vile mbegu, mbolea na fatalaiza ya kuimarisha mazao, na dawa dhidi ya wadudu na magonjwa. Shughuli za kulima, upanzi, palizi na kupulizia dawa yeye ndiye hujifanyia. “Kwa siku nikijilipa leba Sh500 ninasalia na faida ya Sh1, 000. Nimeratibu shamba langu kiasi kwamba halikosi mazao,” anaiambia Akilimali.

Wakati wa mahojiano tulipata amepamba shamba lake kwa spinachi, sukuma wiki, broccoli, mboga za kienyeji – sucha na mchicha. Pia ameanzisha ukuzaji wa mbilingani maarufu kama eggplant, kiungo cha mapishi kinachowiana na matango

“Mvua kubwa inayoendelea kushuhudiwa imesababisha nyanya na pilipili mboga kulemewa na magonjwa yanayojiri kupitia maji mengi,” akasema. Mvua inapokunya kupindukia nyanya na mimea inayoorodheshwa katika familia moja (na ya nyanya) huhangaishwa na maji, yanayosababisha minyanya na mazao kuoza.

Powdery mildew na downy mildew ni magonjwa sugu yanayoathiri minyanya na matunda yake, na yanajiri kupitia baridi na ukungu. “Ili kukabiliana na changamoto za aina hiyo, tunahimiza wakulima kukumbatia mbegu zinazoweza kustahimili magonjwa ya baridi na ukungu,” ashauri Emmah Wanjiru, mtaalamu wa masuala ya kilimo.

Hata ingawa mbegu za aina hiyo ni ghali kwa ajili ya hulka na ustahimilivu wake, mdau huyo anatahadharisha kuwepo kwa mbegu bandia na za hadhi ya chini sokoni. “Wawe makini kuepuka matapeli, kwa kuwa soko limesheheni zile ghushi. Wanunue mbegu za kampuni zilizopigwa msasa na kuidhinishwa na asasi husika,” asisitiza Bi Wanjiru.

Wateja wa Eric Mutunga ni wa kijumla, hususan kina mama wa soko kutoka Ngoigwa na mazingira yake, ikiwamo masoko ya Thika. Ni kupitia kilimo, kijana huyo ameweza kununua pikipiki.

“Mchana huwa shambani na jioni ninafanya kazi ya uanabodaboda,” aeleza. Anaongeza kusema kuwa wateja wake shambani pamoja na wakulima wenza humpa kazi ya kuwabebea mazao, hatua anayosema humuingizia mapato mazuri.

You can share this post!

AKILIMALI: Brokoli, mboga yenye faida kiafya na kimapato

AKILIMALI: Manufaa ya mianzi kwa maisha ya binadamu

adminleo