• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
Wanabodaboda: Hatutashiriki maandamano ya Azimio

Wanabodaboda: Hatutashiriki maandamano ya Azimio

NA MERCY KOSKEI

CHAMA Kinachoangazia Usalama wa Wanabodaboda Nchini kimetangaza kuwa wanachama wake hawatashiriki maandamano ya Azimio. 

Muungano wa Azimio la Umoja, unaoongozwa na Raila Odinga umesema utarejelea maadamano hasa baada ya mfungo wa Ramadhan.

Akizungumza Ijumaa wakati wa kongamano la kila mwaka la viongozi wa bodaboda jijini Nakuru, mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho Bw Kevin Mubadi alisema maandamano hayo yanalenga kuyumbisha nchi.

Aidha, Mubadi alisema kuwa sekta hiyo imewapa ajira mamia ya watu hususan vijana wanaotegemea kutunza familia zao, akielezea kuwa maandamano hayo yanalenga tu maslahi ya watu binafsi na wala si Wakenya kwa jumla.

Wawakilishi wa wahudumu wa bodaboda, walitoka maeneo mbalimbali nchini, Bw Mubadi alisema kuwa kama chama wameamua kufanya kazi na serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto.

Alisema wanabodaboda waliafikia uamuzi huo kwani wamekuwa wakipata msaada kutoka kwa serikali hasa kupitia Wizara ya Masuala ya Ndani na ile ya Uchukuzi.

“Sasa ni zamu yetu ya kushirikiana na Serikali ambayo tumekuwa tukipata msaada, tumetangaza kwamba hakuna mwendesha bodaboda atakayeshiriki maandamano kwani inavuruga nchi yetu ilhali tunategema kazi hii kukimu maisha yetu na familia zetu,” Mubadi alisema.

Mkutano huo ulihudhuriwa na kamanda wa polisi Kaunti ya Nakuru Bw Zachary Kimani, Kamishna wa Kaunti Lyford Kibaara, Meneja wa Mamlaka ya Usalama Barabarani (NTSA) Joseph Gichoi na viongozi wengine wa kaunti katika sekta ya usalama.

Viongozi hao walizungumzia usalama wa waendeshaji bodaboda na pia wateja wao.

Kamishna Kibaara aliwahimza kujiandikisha katika mpango unaoendelea wa kidijitali unaolenga kudhibiti wendeshabbodaboda wanaotumia fursa hiyo kutekeleza uhalifu.

Alisema kuwa wahalifu wamekuwa wakitumia jukwaa la sekta ya bodaboda na kuibia wateja na hata kusababisha.

Hilo, kamishna alisema inahapaka tope wahudumu wa bodaboda na kuchukuliwa kama sekta iliyooza.

Afisa wa Kitengo cha Trafiki Bonde la Ufa, Bi Muleke Mboya alibainisha kuwa asilimia 80 ya mauaji ya barabarani yanayoandikishwa kila siku yanahusisha waendesha bodaboda akisema kila mara wanalaumiwa kuwa kwenye makosa.

Alisikitika kuwa ajali nyingi zinazoripotiwa husababishwa na uzembe wa wahudumu hao, akisema unaweza kuepukwa kwa kufuata sheria za trafiki.

Aliwataka kuvalia vifaa vyao vya usalama kabla ya kuanza safari, ikiwa ni pamoja na kuwa na leseni, bima ya afya na stakabadhi nyinginezo zinazohitajika ili kuepuka mkwaruzano na askari wa trafiki.

“Bodaboda inachangia pakubwa katika ukuaji wa uchumi, japo sekta hii inaandikisha idadi kubwa ya ajali kila siku na asilimia kubwa. Tunataka kubadilisha hili, sote tuwajibike,” alisema.

 

  • Tags

You can share this post!

Wakenya 3 wateuliwa kujiunga na muungano wa madaktari...

Wakora wavamia akaunti za Vyombo vya Habari na kuchapisha...

T L