KRISMASI: Jogoo wa mijini wateka vijiji
Na VALENTINE OBARA
MAELFU ya Wakenya mwaka huu wameendeleza desturi yao ya kuelekea vijijini kwa sherehe za Krismasi licha ya wengi kulalamikia hali ngumu ya kiuchumi.
Kila mwaka, idadi kubwa ya wananchi huchukua likizo kazini katika miji huku kampuni nyingi zikifungwa kwa muda ili wafanyakazi wapate muda wa kujumuika na jamaa zao kwa sherehe za Krismasi na kufungua mwaka mpya.
Wengi huelekea katika mitandao ya kijamii kutangaza yale wanayofanya vijijini, ambapo wakati mwingi huwa wanasambaza picha tele zinazowaonyesha wakiwa katika karamu za mlo na vinywaji vya aina mbalimbali.
Lakini wanapofanya hivyo, kuna wale ambao huwakejeli kwa ziara hizo wakikosolewa kuwa wanaenda vijijini mara moja tu kwa mwaka, ilhali kutembelea jamaa hustahili kuwa jambo linalofanywa mara kwa mara ndani ya mwaka.
Upekuzi kwenye mitandao ya kijamii unaonyesha kwamba, wanaokimbilia vijijini wakati wa msimu huu hufanyiwa utani na wenzao kwa kupeleka tabia zao za mijini mashinani huku wengine wakijitafutia fahari kuu.
“Mojawapo ya changamoto kuu vijijini itakuwa jinsi ya kutupa mikebe ya pombe, chupa za maji za plastiki na chupa za mivinyo. Kutakuwa na tani tele za takataka hizi vijijini wakati mwaka utakapokamilika,” akasema Bw Ted Malanda, ambaye ni mwanahabari jijini Nairobi kwenye mtandao wa Facebook.
Kwa kawaida, vyombo hivi vya vinywaji na mvinyo huwa havipatikani kwa urahisi mashambani.
Vilevile, kunao wanaodai kwamba katika msimu huu, wakazi wa mijini hupeleka misongamano chungu nzima vijijini kwao.
Misongamano hii sio tu barabarani kwa ongezeko la magari ya kibinafsi bali pia katika maduka madogo ya kujipakulia bidhaa ambayo yamechipuka katika baadhi ya vijiji nchini.
Inaaminika huu ni wakati ambapo wamiliki wa maduka hayo watavuna pakubwa kwa sababu waliotoka mijini watataka kuonyesha uwezo wao wa kifedha kwa kununua bidhaa tele zinazohitaji kusukumwa kwenye toroli, licha ya kuwa maduka yenyewe hayana nafasi kubwa.
Pia, wageni hawa wamekuwa wakionywa mitandaoni kwamba wakienda madukani, wasiitishe bidhaa ambazo wanajua wazi zinapatikana tu katika miji mikubwa.
Hawatajionyesha tu katika maduka na bomani bali pia wakienda kuburudika katika mikahawa au baa za vijijini.
Lakini wameonywa kujihadhari dhidi ya wanakijiji watakaokuwa wakiwaita majina makubwa ya kifahari kama vile ‘mheshimiwa’ kwani watajikuta wametumia kiasi kikubwa cha hela kupita kiasi kisha wabaki hoi ifikapo Januari.
“Ukienda kijijini mwezi huu na watu wakuite majina kama vile Ratego (Mzito), Jakom (Mwenyekiti) au Jatelo (Kiongozi), wewe jua tu utakuwa mashakani mwezi ujao,” akasema Bi Omollo Abbah Katey.
Kwa upande wake, mwanahabari Paul J Wafula anashauri watu wawe wakitembelea vijijini mara kwa mara badala ya kusubiri msimu wa Krismasi pekee.
Huku akionyesha picha ya nyumba iliyoharibiwa, alisema kuna baadhi ya wakazi wa mijini ambao watashtuka wakifika vijijini kwa sherehe za Krismasi kwani watakuta nyumba haziko jinsi walivyoziacha.