• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
TAHARIRI: Mwaka 2020 uwe wa heri kwa spoti

TAHARIRI: Mwaka 2020 uwe wa heri kwa spoti

Na MHARIRI

HATIMAYE mwaka wa 2019 umekaribia ukingoni!

Ni mwaka uliokuwa na mema yake, mabaya yake, machungu yake, matamu yake, vilio vyake, vicheko vyake, masaibu yake, baraka zake, pandashuka zake, miteremko yake, malalamiko yake na furaha yake. Hayo ni kawaida katika maisha.

Katika wanda la spoti hayo yote yalijidhihirisha hapa na pale. Tulishuhudia matukio ya kupendeza na wakati mwingine tukakabiliana na machukizi.

Lakini baada ya kuyapitia yote yaliyojitokeza 2019, ni muhimu sasa kuongozwa na methali yaliyopita si ndwele tugange yajayo.

Sharti tupanie kuhakikisha kuwa mwaka wa 2020 unakuwa bora kuliko huu unaopita kuhusiana na masuala ya spoti.

Ni kitu gani tunachoweza kujifunza kutokana na changamoto tulizopitia mwaka huu? Katika kujibu swali hili, ni bora kuangazia kila tatizo katika kila fani ya michezo. Hata hivyo, pia pana matatizo ambayo yanakata kati katika michezo yote.

Fani ya kandanda haikusazwa kwani palishuhudia timu za taifa na klabu zikitatizika sana kutokana na uchechefu wa kifedha; uliotokana hasa na ubadhirifu na ufisadi.

Palikuwapo wakati ambapo kikosi cha Harambee Starlets kilikatiza kambi yake baada ya kukosekana pesa za kufanikisha mazoezi licha ya kuwa kilikabiliwa na mechi ngumu na muhimu ya kimataifa.

Karibu mechi hiyo ifutiliwe mbali kutokana na dosari hiyo.

Pia paliibuka ufichuzi kuwa viongozi wa kandanda nchini walifuja pesa kikosi cha Harambee Stars kilipokuwa nchini Misri kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) ambapo maafisa hao walisemekana kutumia zaidi ya robo tatu ya pesa zilizotolewa kugharimia matumizi ya timu hiyo.

Vilevile, Harambee ilipozuru Misri kwa mechi ya kufuzu kwa Kombe la Afrika la 2021, ripoti za ulaghai wa viongozi waliosafiri na timu hiyo ziliibuka.

Hilo si tatizo linaloathiri soka pekee bali pia katika michezo mingineyo kama vile raga, voliboli, riadha na kadhalika.

Katika riadha pamekuwa na changamoto ya matumizi ya dawa za kututumua misuli (pufya), hali ambayo imeichafulia nchi hii jina pakubwa. Sharti matatizo haya yaepukwe kuanzia mwaka ujao wa 2020.

Lakini la muhimu zaidi ni wadau wakiongozwa na mashirikisho ya michezo mbalimbali kwa ushirikiano na serikali yaweke mikakati bora zaidi ya kuhakikisha viwango vya Kenya vimeimarika ndiposa timu zetu ziweze kufuzu kwa vinyang’anyiro vya Afrika na Dunia.

You can share this post!

Ruto atupia Kalonzo ndoano

FUNGUKA: ‘Mke wa mtu raha tupu’

adminleo