DAU LA MAISHA: Ni miaka saba sasa tangu akitupe kisu cha ukeketaji
Na PAULINE ONGAJI
ALIPOKATA kauli kuachana na kazi ya kukeketa wasichana, bila shaka alitambua kwamba mambo hayangekuwa rahisi hasa ikizingatiwa kwamba uamuzi huo ungeziba mwanya aliokuwa akitumia kujitafutia riziki yake ya kila siku.
Huu ukiwa mwaka wa saba tangu atupilie mbali kisu cha ngariba, Chepongil Ngurianyang, 69, mkazi wa eneo la Morpus, Kaunti ya Pokot Magharibi, anajitahidi kuhakikisha kwamba utamaduni huu wa kale unaangamizwa katika jamii yake.
Amekuwa akitembea katika vijiji vyake kuelimisha jamii na hasa wanawake kuhusu madhara ya ukeketaji sio tu kwa afya ya mhusika, bali pia kwa maendeleo ya kijamii.
Baadhi ya ujumbe ambao amekuwa akieneza ni uhamasishaji kuhusu madhara yanayotokana na shughuli hii. “Kwa mfano, baada ya mafunzo zaidi kutoka kwa shirika la World Vision, nilielewa jinsi ukeketaji una madhara kwa afya ya msichana, vile vile kwa jamii,” aeleza.
Na ni ujumbe huu ambao amekuwa akieneza vijijini ambapo ushawishi wake umeleta mabadiliko katika jamii yake. Kwa mfano, idadi ya wasichana wanaokeketwa katika eneo lake imekuwa ikipungua huku wazazi sasa wakiwapeleka mabinti zao shuleni.
“Idadi ya wasichana ambao wanakamilisha shule na hata kujiunga na vyuo vya masomo ya juu imeongezeka, na hiyo ni fahari kwa jamii yetu,” asema.
Pia, japo Bi Ngurianyang anasema kimekuwa kibarua kigumu kushawishi kila mtu kuhusiana na athari za utamaduni huu uliokita mizizi eneo hili, kwa wale ambao wameshuhudia faida za jitihada zake, wanamchukulia kama jasiri.
Anasema alijifunza kazi hii angali mchanga huku akipokea mafunzo kutoka kwa akina mama kijijini. Kwa hivyo alipofanikiwa kuwa na watoto wasichana, ilitarajiwa kwamba angehakikisha kwamba pia wao wanatahiriwa.
“Mimi ni mama wa watoto kumi; watano wa kike na watano wa kiume. Mabinti zangu watatu wakubwa walipofika umri wa kukeketwa, nilihakikisha kwamba wanafanyiwa hivyo,” aeleza.
Lakini pia ni wakati huu ndipo alipoanza kutambua madhara yanayosababishwa na shughuli hii, suala lililomfanya kuwakinga mabinti zake wawili wa mwisho kutokana na utamaduni huu. “Hawa wawili walienda shuleni na wamekuwa faida kuu kwangu, na hivyo kunifanya niendeleze vita dhidi ya utamaduni huu,” asema.
Lakini haijakuwa rahisi kwani uamuzi huu ulimuacha na pengo kifedha kwani hii ndio iliyokuwa mbinu yake ya kipekee ya kujitafutia riziki. “Kwa mfano kila nilipokuwa nikiitwa kukeketa msichana, ningelipwa pesa, mbuzi na hata pombe, suala lililofanya iwe rahisi kwangu kukidhi mahitaji ya familia yangu,” aeleza.
Aidha, alikuwa akiheshimika sana katika jamii yake ambapo alitambuliwa kote alipokwenda kijijini. Hata hivyo hayo yamebadilika kwani mbali na ukosefu wa pesa kwa njia hii, suala ambalo limemlazimu kutafuta mbinu mbadala za riziki, pia imembidi kuvumilia kutengwa.
“Kama mkeketaji katika jamii hii, unachukuliwa kuwa shujaa. Lakini pindi unapobadili msimamo, huonekana kama msaliti kwani sasa unaenda kinyume na utamaduni wako,” asema, huku akiongeza kwamba hasa amekuwa adui wa waliokuwa wakeketaji wenzake.
Hata hivyo hilo ni tone ikilinganishwa na madhara yanayotokana na ukeketaji. “Kwanza kabisa msichana anapokeketwa, hali yake ya kiafya huathirika ambapo akiwa na mimba inakuwa vigumu kujifungua. Isitoshe, bali na masuala ya kiafya, ukeketaji unahimiza wazazi kuwaoza mabinti zao wakiwa wachanga, kumaanisha kwamba hawaendelei na masomo, suala ambalo limeathiri sana ustawi wa jamii yetu.”
Pia, anazungumzia jinsi uamuzi huu ulivyomsaidia kuacha kunywa pombe. “Kama mkeketaji, mojawapo ya zawadi unazopewa na familia za wasichana ni pombe. Hii inamaanisha kwamba lazima utumie kileo na hivyo mara nyingi hauwezi kumakinika na mambo ya familia yako,” aeleza.
Na sababu hizi anasema ni tosha kumfanya azidishe vita vyake dhidi ya utamaduni huu uliopitwa na wakati.