Habari

Kemikali ya pombe yanaswa kwenye lori la maji

December 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

MAAFISA wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) wakishirikiana na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wamenasa lita 7,500 za kemikali ya ethanol ambayo hutumiwa kutengeneza pombe katika mji wa Sultan Hamud, Kaunti ya Makueni.

Kwenye taarifa iliyotumwa Jumamosi kwa vyumba vya habari, KRA imesema kemikali hiyo ilipatikana imefichwa ndani ya tangi la maji la lita 10,000 kwenye lori.

Bidhaa hiyo haikuwa imelipiwa ushuru wa kima cha Sh2 milioni, kulingana na mamlaka hiyo.

“Baada ya ukaguzi wa kina, ilibainika kuwa lori hilo lilikuwa likibeba lita 2,500 ya maji ndani ya matangi mengi madogo huku tangi la pili likibainika kubeba ‘ethanol’,” KRA ikasema kwenye taarifa hiyo.

“Sampuli zilichukuliwa na kupelekwa kwa ukaguzi katika maabara ya KRA na ile ya Serikali na ikabainika kuwa shehena hiyo ilikuwa ni kemikali hiyo hasa,” taarifa hiyo ikaongeza.

Dereva wa lori na mmiliki wa lori wamekamatwa na watafikishwa mahakamani mnamo Jumatatu kukabiliwa na mashtaka kadhaa ikiwemo la kusafirisha kinyume cha sheria, bidhaa isiyolipiwa ushuru wa kiwango kisichopungua Sh2 milioni.

“Uchunguzi bado unaendelea kuhakikisha kuwa wale ambao walikuwa wanapelekewa kemikali hiyo na washirika wao wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa sheria,” ikaongeza KRA.

Mnamo mwaka wa 2015 mamlaka ya KRA ilichapisha katika vyombo vya habari mwongozo utakaozingatiwa katika ununuzi na uagizaji wa kemikali ya ethanol. Hii ilikuwa ni sehemu ya mkakati wa serikali kudhibiti utengenezaji na utumiaji mvinyo uliotengenezwa kwa kemikali hiyo.

Mwongozo huo, ambao ulianza kutumika mnamo Septemba 1, 2015, pia ulilenga kudhibiti wa matumizi wa ‘ethanol’ na madhara yake, yakiwemo kupotea kwa mapato.