Habari Mseto

Jiji la Nairobi limesakamwa na majitaka, ripoti yafichua

December 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ANITA CHEPKOECH

ASILIMIA 60 ya kinyesi cha binadamu jijini Nairobi haizolewi kwa njia salama, hali inayotishia afya ya wakazi, hasa katika mitaa ya mabanda yenye misongamano ya watu.

Ripoti iliyotolewa na Taasisi ya World Resource Institute (WRI) kuhusu tathmini ya usafi wa kimazingira katika miji 15 mikuu Kusini mwa Jangwa la Sahara, inasema kuwa Nairobi inakabiliwa na uhaba wa miundo mbinu ya kuhakikisha usafi wa kimazingira kwani watu wengi bado wanatumia mbinu duni za kwenda haja kubwa.

“Katika kitongoji cha Kosovo, mtaani Mathare kwa mfano, asilimia 98 ya wakazi bado wanatumia mbinu za duni za kuondoa maji taka,” inasema ripoti hiyo huku ikionya kuwa kero za uchafuzi wa mazingira huenda likasababisha madhara makubwa.

Kando na Nairobi ripoti hiyo kwa jina “Untreated and Unsafe: Solving the Urbanisation Crisis in the Global South” ilikusanya data kutoka miji ya Kampala (Uganda), Lagos (Nigeria), Maputo (Mazambique), Mzuzu (Malawi), Benglaluru (India), Colombo (Sri Lanka), Sao Paulo (Brazil) kati ya miji mingine.

Kulingana na ripoti hiyo ni nyumba chache sana za kibinafsi jijini Nairobi ambazo zimejengwa mashimo ya kuelekeza majitaka huku asilimia 50 ndizo zina miundo mbinu hizo.

Na asilimia 42 ya nyumba za makazi zinatumia vyoo vya shimo, ndoo au wanaenda haja kwenye karatasi za plastiki na kurusha nje kwenye mitaro.

“Ni jambo la kawaida kuona vyoo vilivyojaa kupita kiasi, mabomba ya majitaka yaliyopasuka na vinyesi vya watu walioenda haja mahali wazi. Hali hii inaweza kuchafua maji ya matumizi nyumbani na hivyo kusababisha maradhi hatari, “ watafiti hao wanasema.

Lakini kulingana na ripoti hiyo miongoni mwa miji ambako utafiti huo uliendeshwa, Nairobi ilibainikiwa kuwa na kiwango cha juu cha matumizi ya miundo mbinu ya maji taka ambapo asilimia 45 ya nyumbani zimejengewa mitaro hiyo nje.

Wanasayansi wakuu walioandika ripoti hiyo; David Sathertwaite, Victoria Beard, Diana Mitlin na Jillian Du, wanasema miji inapasa kuhakikisha kuwa imejenga miundo mbinu ya kudumisha usafi wa mazingira katika maeneo yote ya makazi ili kuyafanya kuwa bora kwa watu kuishi.