Habari

Feri iliyosababisha kifo cha mwanamke na mwanawe kutohudumu

January 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MOHAMED AHMED na MISHI GONGO

HATIMAYE shirika la huduma za feri nchini (KFS) limeondoa MV Harambee kuhudumu katika kivuko cha Likoni.

Feri hiyo kuukuu ambayo ilimulikwa baada ya kutokea kifo cha Bi Miriam Kighenda na mwanawe aliyekuwa na umri wa miaka minne Amanda Mutheu imesitisha kuhudumu katika kivuko hicho siku nne tangu amri ya kuondolewa kwake.

Amri hiyo ilitolewa na Waziri wa Usafiri Bw James Macharia baada ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Haji kutoa agizo hilo.

Bw Haji alitoa agizo hilo baada ya kuona bado feri hiyo inahudumu wiki iliyopita licha ya hali yake duni.

Kulitokea sarakasi baada ya Bw Haji na mshirika wake wa karibu mkurugenzi wa uchunguzi wa makosa ya jinai Bw George Kinoti kufika katika kivuko cha Likoni na kushuhudia feri hiyo.

Wawili hao walikuwa wakielekea Golini, Kaunti ya Kwale kuhudhuria harusi ya mkuu wa kitengo cha kupambana na dawa za kulevya Bw Hamisi Masa.

Maafisa katika kivuko cha feri baada ya kufahamishwa ujio wa wawili hao waliandaa MV Harambee kuwavusha wawili hao na msafara wao kuenda Pwani Kusini.

“Msafara wa Bw Haji ulikuwa hapa mchana ambapo walikuwa wakielekea Kusini mwa Pwani lakini baada ya Bw Haji kuona feri hiyo alikataa kuitumia na kudadisi mbona feri hiyo bado ilikuwa inatumika licha ya hali yake mbaya,” akasema afisa mmoja aliyekuwa kituoni hapo.

Inasemekana kuwa Bw Haji alimpigia simu waziri Macharia na kumtaka asimamishe matumizi ya feri hiyo mara moja.

“Baada ya simu hiyo, taarifa ikaja kwa meneja mkurugenzi wa huduma za feri kuondoa feri hiyo isihudumu,” afisa mmoja katika shirika hilo akasema.

Feri hiyo ilimulikwa Septemba 29, 2019, baada ya gari la Bi Kighenda na mwanawe Amanda kuchomoka kutoka ndani ya feri hiyo na kutumbukia baharini na miili yao kupatikana siku 13 baadaye.

Baada ya tukio hilo uchunguzi ulianzishwa dhidi ya usalama wa feri hiyo. Hata hivyo, ilionekana kuwa uchunguzi huo haukuzaa matunda ambapo feri hiyo iliendelea kuhudumu licha ya hali yake mbaya.

Katika uchunguzi wa kamati ya bunge, ilifichuka kuwa mamlaka ya bahari nchini ilipeana vibali vya uhudumu wa feri hizo bila ya kuzifanyia ukaguzi.

Shirika hilo lililaumiwa kwa kupeana kibali kwa feri hiyo licha ya nanga zake kuwa mbovu.

Ubovu huo ndiyo uliohusishwa na vifo cha Bi Kighenda na mwanawe ambavyo vilitetemesha nchi na hata dunia nzima.

Feri hiyo ni miongoni mwa nyingine tatu ambazo seneti imetaka ziondolewe katika shughuli za usafiri.

Nyingine ni MV Kilindini na MV Nyayo ambazo zimekuwa zikihudumu kwa zaidi ya miaka 30 sasa.

Usitishaji wa kuhudumu kwa feri hizo unatarajiwa kupewa kipaumbele bunge litakapofunguliwa kwa majadiliano mwaka 2020.

Feri hizo zikisimamishwa kuhudumu shirika hilo litasalia na feri tatu pekee kivukoni ambazo ni MV Jambo, MV Kwale na MV Likoni.

Kusitishwa kwa feri hizo kutasababisha msongamano katika kivuko cha Likoni.

MV Likoni inatarajiwa kuhudumu katika kivuko cha Mtongwe ambacho kwa sasa kinafanyiwa ukarabati.

Kwa kawaida saa ambazo kuna abiria wengi feri tano au nne huhudumu katika kivuko cha Likoni ambazo huweza kudhibiti umati huo.

Hata hivyo, shirika hilo limeweka matumaini yake kwa ujio wa feri mpya; MV Safari ambayo inatarajiwa kufika nchini katikati ya Januari 2020.