Habari Mseto

Magogo ya miti iliyosombwa na maji yalemaza shughuli ya kuwafikia wahasiriwa wa mafuriko Tana River

January 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MISHI GONGO

SHIRIKA la Msalaba Mwekundi nchini linasema magogo yanatatiza juhudi za kuwafikia wahasiriwa wa mafuriko Kaunti ya Tana River.

Magogo hayo ambayo ni ya miti iliyosombwa na maji kufuatia mafuriko yanayoendelea kaunti hiyo, yanatatiza usafiri wa mashua ambazo zinatumika kupeleka msaada maeneo mbalimbali yaliyoathirika.

Akizungumza na ‘Taifa Leo’ kwa simu, meneja wa shirika hilo katika ukanda wa Pwani Bw Hassan Musa, amesema maafisa wa shirika hilo wanalazimika kusitisha safari mara kwa mara kuondoa magogo makubwa yanayosiba njia yao ya majini.

“Tunapata wakati mgumu kufikia baadhi ya maeneo kwa sababu magogo yanazuia mashua. Kufikia sasa tumefikia asilimia 90 ya eneo la Tana River na kubakisha asilimia 10. Sehemu zilizosalia ziko na changamoto za kuzifikia sababu ikiwa ni hali mbaya ya njia,” akasema Bw Musa.

Meneja huyo amesema tayari wamefikia nyumba 1,222 eneo la Tana Delta na nyumba 1,219 eneo la Tana Kaskazini.

“Sehemu zilizoathirika zaidi na ambazo tumezifikia ni Handaraku, Kikomo, Marafa Camp, Odole Camp, Samicha, Kiembeni, Korlabe A,B na C, Tawakal, Escedec, Tara, Bura Anani, na Ongonyo. Maeneo ya Tana Kaskazini tumefika Adele, Madogo, Sala, Didha, Taleo, Billi Sombo, Gora, Gubatu na vilevile Anole A na B,” akasema Bw Musa.

Bw Musa alisema kuwa wanaendelea kuzunguka maeneo hayo kugawanya vyakula na bidhaa zingine kusaidia familia zilizokutwa na mkasa.

“Tumewafaa kwa vyakula, neti za mbu, mashuka na bidhaa zingine kwa maeneo yaliyoathirika zaidi. Hata hivyo, magogo ambayo yamesombwa na maji yamekuwa yakilemaza juhudi zetu za kufikia baadhi ya maeneo,” akasema.

Bw Musa amewarai Wakenya kuwasaidia wakazi wa eneo la Tana.

Alieleza kuwa baadhi ya wakazi wamekwama katika vijiji vyao kufuatia mafuriko hayo.

Aliongeza wakazi hao wanahitaji msaada kwani wengi wao wamepoteza nyumba zao, wanyama na hasa mifugo.

Pia alisema wanahofia mkurupuko wa maradhi kufuatia mafuriko hayo.

Mafuriko hayo yalitokea baada ya mvua iliyopitiliza iliyokuwa ikishuhudiwa nchini kuanzia Oktoba 2019 na ambayo ilisababisha Mto Tana kuvunja kingo zake.

Aidha alisema mikakati inafaa kuwekwa kuhakikisha kuwa hali hiyo inatatuliwa kuhakikisha maafa haya hayatashuhudiwa tena miaka ijayo.