• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 1:13 PM
MATUKIO YA 2019: Mafuriko yalivyotatiza wakazi Thika

MATUKIO YA 2019: Mafuriko yalivyotatiza wakazi Thika

Na SAMMY WAWERU

MWAKA wa 2019 uliofika tamati Jumanne ulikuwa wenye matukio tofauti, kuanzia kamatakamata ya washukiwa wa sakata za ufisadi, mauaji ya kiholela yaliyohusisha masuala ya ndoa na uchumba, ukame na hata mafuriko.

Licha ya ukame ulioshuhudiwa mwaka huo katika baadhi ya maeneo nchini, kipindi cha lala salama hususan mwezi Novemba na Disemba kilishuhudia mvua ya mafuriko, iliyosababisha maafa ya watu na mifugo, nyumba na mazao ya kilimo kusombwa na kasi ya maji.

Isitoshe, mamia walilazimika kuhama wanakoishi kwa ajili ya nyumba zao kuzingirwa na hata kufunikwa na maji, hasa kaunti ya Kisumu.

Katika muktadha uo huo wa mvua ya gharika, maeneo mengine yasingepitika kwa sababu ya barabara kufurika na hata madaraja ya kusombwa. Eneo la Thika lilikuwa miongoni mwa yaliyoathirika. Katika mtaa wa Tola, daraja linalounganisha eneo hilo na Thika, lilifurika maji jambo lililotatiza shughuli za usafiri na uchukuzi.

Daraja hilo pia liliharibika, kutokana na mvua ya mafuriko iliyoshuhudiwa maeneo mbalimbali nchini.

Mto Tola ulifurika na kufuja kingo zake, kiasi cha maji kuelekeza mkondo wake katika makazi. Baadhi ya nyumba zilizo karibu, zilizingirwa na maji jambo ambalo lilizua hatari kwa wanaoishi humo.

Kulingana na wakazi, hali hiyo ilishuhudiwa kwa muda wa zaidi ya wiki mbili. “Wengi hawakuenda kazini kwa sababu ya kukosa mahala pa kupitia, daraja tunalotumia maji yalifurika,” akalalamika mhudumu wa bodaboda na mkulima, Eric Muli,  wakati wa mahojiano na ‘Taifa Leo’.

Licha ya kupata afueni, miamba ya mawe kumwagwa kwenye daraja hilo ili kupunguza kasi ya maji, wakazi walihofia mvua ikiendelea huenda hali ikawa tete zaidi.

“Tunaona kiwango cha maji kikiendelea kuongezeka na hata kufunika mawe yaliyomwagwa,” akasema Bw Mutunga.

Wapita daraja walionekana kujawa na wasiwasi, hasa kwa sababu ya miamba iliyomwagwa kwani haijasitiriwa na chochote. Isitoshe, ni eneo lenye watoto na ambao wakati wa mahojiano walionekana wakivuka.

Katika baadhi ya mashamba eneo hilo, wakulima wanakadiria hasara bin hasara kufuatia mimea na mazao kusombwa na maji. Wakulima tuliozungumza nao, walisema hali iliyoshuhudiwa huenda ikasababisha taifa kukumbwa na ukosefu wa chakula mwaka huu, 2020.

“Hata ingawa shamba langu halijaathirika sana, mambo yakiendelea ninavyoona taifa litakosa chakula mwaka 2020,” akaonya Irene Wanjiru.

Mbali na Tola, Ngoingwa, Makongeni, Kiganjo na Munyu, ni maeneo yaliyoathirika kwa mafuriko ya mvua. Kwa mfano, Soko la Makongeni, halikuwa likiingilika sawa na eneo la Munyu ambapo barabara ni mbovu.

Idara ya utabiri wa hali ya hewa ilibashiri kuwa mvua itaendelea hadi mwishoni mwa Desemba 2019.

Takwimu zinaonesha mafuriko hayo yalisababisha maafa ya zaidi ya watu 100, mamia kusalia bila makao na hasara ya mali.

You can share this post!

UANDISHI: Mathias Momanyi ni mwandishi mahiri wa vitabu vya...

AKILIMALI: Wana mimea-dawa ya ubora wa juu uliowapa soko...

adminleo