‘HATUNA KIFANI’: Liverpool yachapa Sheffield United 2-0
Na MASHIRIKA
LIVERPOOL, Uingereza
KOCHA Jurgen Klopp alikuwa mwenye furaha tele baada ya vijana wake wa Liverpool kuchapa Sheffield United 2-0 siku ya Alhamisi na kumaliza miezi 12 bila kupoteza katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Liverpool, ambayo mara ya mwisho kupoteza ligini ilikuwa Januari 2019, ilipochapwa 2-1 na mabingwa watetezi Manchester City, imedumisha mwanya wa alama 13 juu ya jedwali.
Ilivuna ushindi dhidi ya Sheffied kupitia mabao ya Mohamed Salah na Sadio Mane uwanjani Anfield.
Vijana wa Klopp sasa wameshinda mechi 19 kati ya 20 ambazo wamesakata ligini msimu huu, wakipoteza alama mbili pekee kwa kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Manchester United mnamo Oktoba 20 mwaka jana.
Tangu walemewe na City ya Pep Guardiola mnamo Januari 3, 2019, Reds hawajapoteza mechi 37 kwenye ligi. Wako mbioni kutawala ligi kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30.
“Hii ni ishara kwamba kuna mambo mazuri tunafanya. Nimekosa hata maneno ya kuelezea mchezo wetu, hatuna kifani,” alisema Klopp.
“Nimejawa na furaha sana; najivunia vijana wangu. Hatufai kupuuza ufanisi kama huu!”
Washindi hao wa mataji 18 ya ligi sasa hawajapoteza mechi 51 ligini, katika uwanja wao wa nyumbani wa Anfield tangu Aprili 2017.
Ushindi dhidi ya Sheffield unafikisha mechi tano mfululizo ambazo Liverpool imeshinda katika EPL msimu huu bila kufungwa bao, mara yao ya kwanza tangu 2007. Dhidi ya Sheffield, Liverpool pia iliweka rekodi yake ya pasi kamilifu 874 hapo Alhamisi.
Manchester City inashikilia rekodi ya pasi za uhakika kwenye EPL ilipoandikisha 942 dhidi ya Swansea mnamo Aprili 2018.
“Jinsi tulivyodhibiti Sheffield United ilikuwa safi kabisa. Kwa umilikaji wa mpira, tulikuwa wazuri sana. Tulikuwa watulivu, lakini pia kuendesha shughuli zetu kwa msisimko. Mabao yalikuwa matamu,” alieleza Klopp baada ya mechi.
“Bila shaka ni kitu kizuri (kumaliza mwaka bila kupoteza ligini), lakini lengo letu halikuwa hili, bali kuvuna ushindi. “Hatuweka akilini mwetu kwamba tumekamilisha mwaka bila kushindwa. Malengo yetu ni ya msimu wala si mipango ya Mwaka Mpya!”
Baada ya mwaka 2019 kushuhudia Liverpool ikitawazwa wafalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Klabu Bingwa Duniani (Club World Cup), lengo lao sasa ni kumaliza utawala wa miaka miaka miwili wa mabingwa watetezi Manchester City. Liverpool ilikosa pembamba ubingwa wa ligi msimu uliopita.
Vijana wa Klopp wamekuwa katika fomu ya kutisha, na sasa watahitaji kuepuka kichapo katika mechi 13 zijazo ligini, ili kufuta rekodi ya mechi 49 ambayo kikosi cha Arsenal, almaarufu Invincibles, kiliweka msimu wa 2003-2004.
Baada ya kuchapa Sheffield, Liverpool inaongoza kwa alama 58 ikifuatiwa na Leicester (45), Manchester City (44), Chelsea (36) na Manchester United (31) katika nafasi tano za kwanza. Arsenal, ambayo itaalika Liverpool uwanjani Emirates mnamo Mei 2, inapatikana katika nafasi ya 10 kwa alama 27.