Makala

MAKALA MAALUM: Amehatarisha maisha yake mara nyingi kutetea haki za wanyonge

January 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 4

Na KALUME KAZUNGU

AMEJITOLEA kwa hali na mali ikiwemo kuhatarisha maisha yake na pia ya familia, ili kutetea haki za wanyonge.

Kutana na Bw Is’haq Abubakar Khatib, mtetezi wa haki za binadamu na pia afisa msimamizi wa shirika la kutetea maslahi na maendeleo ya wenyeji wa Lamu na Pwani, la Lamu Coastal Indigenous People’s Rights for Development (LCIPRD).

Kila unapomuona uso wake huwa umejaa tabasamu. Aghalabu si rahisi kumpata akiwa na sura iliyokunjamana.

Khatib alizaliwa katika kisiwa cha Manda, Kaunti ya Lamu, takriban miaka 39 iliyopita. Kisha akalelewa na nyanyake eneo la Malindi, Kaunti ya Kilifi.

Katika utoto wake, Khatib asema marehemu babake, Abubakar Khatib, alikuwa akimhimiza kutenda mema, kuthamini haki na kutetea ukweli wakati wote maishani mwake.

Babake alikuwa mwanajeshi wa kikosi cha majini cha Kenya Navy.

Punde alipomaliza masomo yake ya sekondari katika shule ya upili ya wavulana ya Lamu Bujra mnamo 2000, alianza kupata mvuto nafsini mwake wa kutetea masuala ya jamii.

Msukumo

Mshawasha huo ndiyo ilimsukuma kujiunga na Chuo Cha Ufundi Anuwai cha Mombasa Polytechnic, ambako alisomea kozi ya Masuala ya Ustawi wa Jamii. Baada ya kuhitimu masomo yake ya chuoni, Khatib alirudi Lamu na kuanza kufuatilia mambo yaliyokuwa yakiathiri jamii ya hapo ya Waswahili ya Bajuni.

Anasema dhuluma za kihistoria zilizokuwa zikiendelezwa dhidi ya jamii yao na vile vile jamii nyingine za ukanda wa Pwani na nchini Kenya kwa jumla, zilimwasha moto ndani mwake kukabili mamlaka za usimamizi.

Dhuluma hizi, aeleza, ni pamoja na unyakuzi wa ardhi, ubaguzi wa serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo katika baadhi ya maeneo, na vile vile ubaguzi katika uteuzi wa wawakilishi serikalini.

Hizi zilikuwa miongoni mwa mambo yaliyomtia mori ya kuwa mpiganiaji wa wanyonge.

Ni kazi ambayo aliianza mnamo 2002 muda mfupi baada ya kuhitimu masomo yake ya chuo.

Ni mmoja wa wanaharakati waliokuja pamoja na kubuni Muungano wa Vijana wa Lamu, almaarufu Lamu Youth Alliance ambao ni miongoni mwa makundi ya kutetea haki za wakazi yanayowasha moto wa mageuzi katika Kaunti ya Lamu.

Mnamo 2009, Khatib na wengine waliafikia kuja pamoja na kuunda vuguvugu la Mashirika ya Kutetea Haki za Binadamu na Mazingira eneo la Lamu, linalotambulika kama Save Lamu.

Ni kupitia muungano huo ambapo Khatib alijizolea umaarufu zaidi ndani na nje ya kisiwa cha Lamu akiwa mwanachama.

Kupitia Save Lamu, Khatib amekuwa akishirikiana na wengine kuandaa makongamano ya kuhamasisha wakazi wa kisiwa hicho jinsi ya kufahamu na kutetea haki zao za kimsingi.

Muungano huo pia umeandaa maandamano kadhaa mjini Lamu na pia jiji kuu Nairobi, katika harakati za kushinikiza serikali kuzingatia matakwa ya wananchi wa Lamu na pia msimamo wao kuhusiana na miradi mbalimbali inayotekelezwa eneo hilo.

Ikumbukwe kwamba katika makongamano au maandamano yoyote yanayoandaliwa ndani na nje ya Lamu, hutamkosa Khatib akiongoza washirika katika kushinikiza serikali kusikiliza malalamishi ya wakazi.

“Nashukuru kwamba tangu nilipoamua kujitosa katika ulingo wa kutetea haki za wanyonge, wakazi wa Lamu wameweza kusikizwa na serikali. Ninafurahi kwamba angalau kwa mara ya kwanza katika historia, wakazi wa Lamu wamepewa hatimiliki za ardhi zao.

“Dhuluma za kihistoria pia zimekuwa zikiangaziwa na marekebisho kufanywa. Serikali pia imetambua haki za wakazi wa maeneo ambayo inatekeleza miradi yake, kwa kuhakikisha waathiriwa wanapewa fidia. Haya ni baadhi ya mambo ambayo tumeyapigania kupitia shughuli zetu za uanaharakati,” akasema Khatib katika mahojiano ya makala haya.

Safari yake ya kuwa mwanaharakati wa kutetea haki za wanyonge haijakuwa rahisi kama inavyodhaniwa.

Vitisho

Khatib anaeleza jinsi amekuwa akipokea vitisho kutoka kwa maafisa wa usalama na hata watu wasiomjua, wanaomshinikiza kuachana na azma yake.

Anasema licha ya vitisho hivyo, bado ataendelea kupigania haki za kimsingi za wakazi wa Lamu na katu hatalegeza kamba.

Mnamo Mei 25, 2018, Khatib na mwenzake ambaye ni Katibu Mkuu wa Save Lamu, Bw Ahmed Walid, walikamatwa na polisi katika kisiwa cha Lamu wakati wakiongoza maandamano ya kupinga kuanzishwa kwa mradi wa nishati ya makaa ya mawe.

Mradi huo wa gharama ya Sh200 bilioni unanuiwa kujengwa eneo la Kwasasi, tarafa ya Hindi, Kaunti ya Lamu.

Makundi mbalimbali ya wanaharakati wa mazingira na kijamii, Walid na Khatib wakiwa mbele kuongoza maandamano hayo tangu mwanzo mradi ulipochipuka, wamepinga ujenzi wake wakisema ni sumu kwa mazingira na afya ya wakazi.

Shinikizo hizo zilizaa matunda baada ya Jopo Maalum la Kushughulikia Masuala ya Mazingira kusitisha leseni ya ujenzi wa kiwanda hicho mnamo Juni 26, 2019.

Hata hivyo, kampuni inayosimamia ujenzi huo, Amu Power imekata rufaa dhidi ya uamuzi wa jopokazi hilo.

“Nimekamatwa mara kadhaa, kupigwa vita na hata kutishiwa maisha ili niache azma yangu ya kutetea haki za wanyonge. Licha ya yote, mimi sitarudi nyuma.

Nimejitolea na nitaendelea kupigania haki za wasiojiweza, kama nilivyopokea wosia kutoka kwa marehemu babangu,” Khatib aliambia Taifa Leo.

Kutokana na harakati zake, shirika la National Coalition for Human Rights Defenders-Kenya (NCHRD-K) lilimtunuku taji la mpiganiaji bora wa haki za binadamu nchini wa mwaka 2018.

“Mimi ndiye mpiganiaji bora wa haki za binadamu nchini 2018. Shirika la NCHRD-K lilinipa utambuzi huo Desemba mwaka jana. Nafurahi sana nikiona haki za binadamu, hasa wanyonge, zinaheshimiwa nchini na ulimwenguni kote kwa jumla,” akasema.

Wosia wake kwa asasi za serikali ni kwamba zihakikishe wanaharakati wa haki za binadamu na raia wanaheshimiwa na kusikizwa wanapowasilisha malalamishi kwao.

Khatib anasema ni kupitia kwa njia hiyo ya mapatano ambapo jamii zinaweza kupata suluhisho la matatizo wanayolalamikia, na hivyo kuwezesha taifa kwa jumla kupiga hatua zaidi kimaendeleo.

“Ningeomba serikali kuhakikisha wanasikiza vilio vya raia na wanaharakati. Hakuna binadamu wa akili timamu ambaye ataamua kuandaa maandamano bila ya sababu. Ni vyema kusikiliza matatizo ya kila mmoja hata yule wa ngazi ya chini kabisa, na kuhakikisha matatizo yake yanasuluhishwa. Hilo likizingatiwa, Kenya itatambulika ulimwenguni kote kwa kuwa nchi ya amani, maendeleo na inayozingatia haki za raia wake,” aeleza afisa huyo msimamizi wa LCIPRD.

Aidha anawashauri vijana kuzingatia dini, kudumisha amani na kutia juhudi maishani ili kuafikia maendeleo ya nchi.

“Vijana wenzangu ninawashauri kujitahidi kutenda yaliyo mema maishani na kuepuka kujiingiza katika makundi ya uhalifu na pia matumizi ya dawa za kulevya. Hayo ni mambo ambayo hayana faida yoyoye kwa mja,” akasema Khatib.