Makala

KINAYA: 'Ouru' ajitokeze kimasomaso na kueleza atang’atuka 2022 au la

January 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DOUGLAS MUTUA

KARIBU mwaka huu mpya wa visanga, vituko na sarakasi.

Ongeza kelele kwenye orodha hiyo. Bila shaka, hizo zitakuwa nyingi kupindukia.

Kisa na maana ni kwamba, tunaendelea kukaribia mwaka wa 2022 ambapo uchaguzi mkuu utafanyika.

Kwani uchaguzi mkuu una nini? Si utafanyika tu, washindi wale vinono, washinde wale huu na hasara juu?

Ndio, ila ni uchaguzi wa aina yake, yaani wa kipekee kabisa. Vipi kwani? Mwenyeji wa sasa wa Ikulu anastaafu mwaka huo, hivyo hatarajiwi kupania kusalia humo.

Hilo ni jumba la umma, ukistaafu unafunganya na kuelekea ulikotoka. Hamna mlala Ikulu asiye na kwake, hivyo hiyo haiwi shida hata kidogo.

Kelele ambazo nimekuahidi kusikia mwaka mzima ni kati ya vijana na wazee. Mwenyeji wa sasa wa Ikulu atakuwa msikilizaji mkuu kwani zinamhusu yeye mwenyewe.

Binafsi, namuomba afyate kabisa ili kelele ziendelee mpaka mwisho. Kwa faida gani? Uhondo wa burudani. Mwenzako napenda kucheka na kuchekeshwa hasa na mambo ya kijinga ambayo hayanikoseshi usingizi.

Tayari umewasikia wazee wakisema eti ‘Ouru’ hatakwenda popote baada ya uchaguzi wa 2022, kwamba lazima apate wadhifa mkuu kama mmoja wa watawala wa nchi.

Wazee wanadai ‘Ouru’ atakuwa kijana mdogo sana wakati huo, eti kumsindikiza hadi kijijini Ichaweri akavune kahawa ni kuwaonea vijana na kuwadharau wazee.

Hivi nani kasema haya? Kikongwe Noah Mahalang’ang’a Wekesa, ambaye Agosti mwaka huu atagonga miaka 84!

Nani mwingine? Hata kidomodomo wa Muungano wa Vyama wa Wafanyakazi (COTU) anayependa kujiita Ndugu Atwoli ameshikilia uzi uo huo.

Huyo naye ana umri wa miaka mingapi? Anasema atatimiza miaka 70 mwaka huu, lakini nahisi kama ni zaidi. Kumbuka kuna nyakati ambapo Afrika miaka haikuhesabiwa, ungejiandikia yoyote tu ukichukua kitambulisho.

Nadhani nimemwona au kumsikia Atwoli tangu nizaliwe, na mwenzako siwi wa jana, chumvi nimekula kiasi cha haja.

Atwoli amesema nguvu alizo nazo ‘Ouru’ zitaharibika bure akiruhusiwa kustaafu, eti aachwe akae nasi hata ikiwa atataka kuwa Waziri Mkuu.

Utadhani umri pekee, na wala si wingi wa kura, ndio mwamuzi wa nani atawale nani! Utadhani hatuna vijana wa kweli wanaoweza kuongoza nchi.

Ikiwa mzee wa miaka 60 anaweza kuitwa kijana, basi naomba niruhusiwe kurarua cheti changu cha kuzaliwa, ichukuliwe kwamba bado sijazaliwa.

Kudai mzee wa miaka 60 aliyejaza mvi kichwani ni kijana barobaro ni ama kuwatukana vijana wa kweli makusudi, au kutumia akili kama kofia.

Ni kuwadhihaki watumishi wa umma wanaostaafishwa wakiwa na miaka 55 au 60, kisha wanalazimika kusubiri hadi watimize miaka 65 ili waanze kupokea malipo yao ya uzeeni.

Tatizo ni kwamba, huwezi kumhukumu mtu aliyeshindwa kutumia akili zake. Kumbuka akili si mpira eti uzivute zirefuke; ukomo wake ukifika basi!

Kenya haina upungufu wa vijana wenye akili timamu. Watakuja juu na kuwaambia wazee wawakome mara moja!

Kwa bahati mbaya, labda matamanio ya Atwoli na Wekesa ni ya kweli; iwe wamevujisha tu siri za watu. Labda tunapaswa kuwashukuru badala ya kuwakejeli.

 

[email protected]