DIMBA: Tierney, ‘ball boy’ aliyegeuka nguli
Na GEOFFREY ANENE
ALIKUWA mmoja wa watoto wa kuokota mpira uwanjani (ball boys) wakati Celtic ilishangaza Barcelona 2-1 kupitia mabao ya Victor Wanyama na Tony Watt kwenye Klabu Bingwa Ulaya mwaka 2012.
Huyu si mwingine, bali ni beki wa pembeni kushoto wa klabu ya Arsenal, Kieran Tierney aliyetokea Celtic kwa Sh3.3 bilioni mwezi Agosti 2019.
Chipukizi huyu ametoka mbali kabla ya kufikia kiwango cha kutambulika katika ulimwengu wa soka.
Kieran, ambaye alizaliwa katika kisiwa cha Isle of Man yapata miaka 22 iliyopita, aliwekewa msingi wa soka na babake Michael na mamake Gail. Wazazi wake ni mashabiki wakubwa wa Celtic nchini Scotland.
Alilelewa jijini Edinburgh, Scotland. Kitindamimba huyu mwanzoni aliharibiwa na wazazi wake akipata chochote alichoitisha kabla ya kuwekewa mipaka.
Kutokana na wazazi wake kuwa mashabiki sugu wa Celtic (walinunua tiketi za kila msimu za klabu hiyo), Kieran alifuata nyayo zao. Aliamua kuwa mwanasoka baada ya Celtic kunyakua mataji mawili – ubingwa wa Ligi Kuu ya Scotland na kipute cha League Cup. Alipenda sana kuenda shuleni kwa sababu kazi ya mamake aliajiriwa kusimamia shughuli za watoto wakati wa kula katika shule aliyosomea.
Hata hivyo, kitendo kilichomsukuma kabisa katika soka ni mwalimu kumuambia awe seremala akiwa mkubwa.
Alipoulizwa na mwalimu huyo katika shule ya msingi kuwa angependa kufanya kazi gani atakapokuwa mkubwa, Kieran alisema mchezaji wa soka ya kulipwa. Hata hivyo, mwalimu alimtaka awazie kuwa seremala wa kuunganisha vitu kama milango, fremu za madirisha na vijidaraja vya kupandia kwenye nyumba.
Alikataa pendekezo la mwalimu kabisa na akaapa kutimiza ndoto yake ya kuwa mwanasoka.
Kieran kisha alijiunga na shule ya upili ya Ninian’s ambayo iliendesha akademia yake kwa ushirikiano na Celtic.
Bidii yake uwanjani ilishuhudia akiitwa na akademia ya Celtic kufanyiwa majaribio akiwa na umri wa miaka saba.
Alipita majaribio hayo vizuri sana. Alichezeshwa mara nyingi kama winga wa kushoto. Vilevile, alifanya majukumu ya watoto wa kuokota mpira uwanjani.
Aliendelea kukomaa, ingawa alipata ugumu kuonekana alipofika umri wa miaka 14. Pia, alipata pigo wakati huo alipovunjika mguu mnamo Desemba 2014 saa chache kabla ya kujumuishwa katika kikosi cha kwanza cha Celtic. Hakufa moyo.
Alisalia na matumaini makubwa kuwa atarejea kwa kishindo.
Alianza kusakata soka ya watu wazima mwaka 2016 na bidii yake ikashuhudia akitwikwa majukumu ya nahodha msaidizi. Kufikia umri wa miaka 20, Kieran alikuwa ameshinda mataji kadha yakiwemo manne ya Ligi Kuu.
Aanza kung’ang’aniwa
Alianza kung’ang’aniwa na klabu kubwa nje ya Scotland alipoonyesha mchezo mzuri kwa kuwakaba mshambuliaji matata chipukizi Kylian Mbappe wa Paris Saint-Germain, gunge wa Bayern Munich Arjen Robben na nyota wa Manchester City Raheem Sterling pamoja na kufunga bao dhidi ya Manchester City kwenye Klabu Bingwa Ulaya msimu 2018-2019.
Mashabiki wengi nchini Uingereza walianza kutamani kuona Kieran akifuata nyayo za beki wa Liverpool Virgil van Dijk na kiungo wa Tottenham Wanyama, ambao walitua katika Ligi Kuu ya Uingereza wakitokea Celtic.
Haikuwa muda kabla ya Kieran kusaini kandarasi ya miaka mitano uwanjani Emirates.
Ingawa mashabiki wa Arsenal hawajapata kuona beki huyu wa Scotland katika mechi nyingi kutokana na majeraha ya kinena ama bega, amewafurahisha kiasi cha kudai kuwa “hakuna beki bora kwenye Ligi Kuu ya Uingereza kama yeye” katika mechi chache alizocheza.
Kieran, ambaye anapokea mshahara wa Sh7.6 milioni kila wiki, anachumbia mwanadensi Amy Hale kutoka Jamhuri ya Ireland.