Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Mwingiliano wa Kiswahili, Kibantu

January 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na WANDERI KAMAU

KATIKA jumla ya masuala yanayohusu lugha ya Kiswahili, hasa uhusiano wake na lugha zingine, uhusiano uliopo baina yake na lugha za Kibantu ndilo limewahi kujadiliwa na wanaisimu mbalimbali kwa marefu na mapana.

Hata hivyo, kuna haja ya kutathmini kwa kina mwoano wa Kiswahili na lugha za Kibantu. Je, undani wa mwoano huu ni upi? Ulifikia wapi?

Katika taaluma ya isimu ya lugha za Kiafrika, na hasa lugha za Kibantu, msomi wa kwanza na anayejulikana sana kutokana na utafiti wake wa miaka mingi katika lugha hizo alikuwa Wilhelm H.I. Bleek.

Katika uainishaji wake wa makundi ya lugha za Kibantu, Bleek (1862) aliiweka lugha ya Kiswahili katika kundi la ‘Zangi’, kundi la kaskazini-mashariki, ambalo kwa mujibu wa utaratibu alioufuata, lilikuwa ni kundi mojawapo kati ya makundi ya Tawi la Kati la Lugha za Kibantu.

Bleek alionesha dhahiri kuwa lugha ya Kiswahili ilikuwa na sifa zake kuu zilizopatikana katika lugha nyingine za Kibantu kwa jumla.

Kauli ya Bleek

Ama kwa hakika, ndiye msomi wa kwanza kudhihirisha kwamba lugha zote za Kibantu zilikuwa na mfumo wa ngeli na ule wa vitenzi ambao ni ambishi bainishi.

Msomi mwingine aliyefuata ni Carl Meinhof. Mchango wa msomi huyu ni kuwa kinyume na Bleek, alizama zaidi katika maelezo.

Kwenye kitabu chake, ‘Introduction to the Phonology of the Bantu Languages’ (1932), Meinhof anachukua msimamo sawa na mtangulizi wake Bleek, kwamba Kiswahili ni Kibantu.

Baada ya Meinhof, kulikuwa na wasomi kama C.M Doke (1935, 1945) na wengine waliojitokeza na ambao kazi zao zilidhihirisha kuwa Kiswahili ni lugha ya Kibantu.

Lakini aliyeibuka maarufu sana na aliyeenda kuwapiku wengine wote ni Malcom Guthrie.

Tathmini ya Guthrie

Katika majuzuu yake yote yanayoitwa Comparative Bantu (1967, 1970, 1970 na 1971) na yenye kurasa zisizopungua 800, kwa pamoja, Guthrie anazitalii lugha nyingi sana za Kibantu na anajaribu kupendekeza lugha ya Mame-Bantu.

Hii ni lugha ya kufikirika ambayo tunaweza kuchukulia kuwa ndiyo iliyozaa lugha nyingine za Kibantu. Katika kazi zake hizo, Guthrie anajaribu kupendekeza hiyo lugha ya Mame-Bantu ilikuwa lugha yenye sura gani na ni mahali gani ambapo pengine ndipo chimbuko la Wabantu wa asili. Mbali na majuzuu hayo makubwa, Guthrie aliandika vitabu vingine vingi juu ya lugha za Kibantu.

Katika uainishaji wake, Guthrie anazigawa lugha hizo katika kanda zenye makundi makubwa mbalimbali kwa mujibu wa maeneo yake ya kijiografia.

Lugha ya Kiswahili inaangukia katika katila kanda G10 na imepewa kitambulisho cha G42.

Ni wazi kwamba kuna mambo kadhaa ambayo wasomi waliofuatia hawakukubaliana na Guthrie, kama ilivyo kawaida ya wasomi wote, lakini kati ya mengi ambayo walikubaliana naye bila kusita ni kule kujumuisha lugha ya Kiswahili katika kundi kubwa au familia ya lugha za Kibantu.

Baada ya Guthrie, kumekuwa na vuvumuko la wasomi wanaojishughulisha sana na lugha za Kibantu na ambao kwa kweli haiwezekani kuwataja wote.

Lakini kwa upande wa historia ya lugha ya Kiswahili, itakuwa si haki kuacha kuwataja Dereck Nurse na Thomas Spear, ambao katika kitabu chao ‘The Swahili: Reconstructing the History and Language of an African Society’, 800-1500 (1985) wanatoa mchango mkubwa sana kuhusu historia ya lugha ya Kiswahili na Waswahili wenyewe.

Nurse na Spear wanalijadili suala hilo kwa ufupi, lakini kwa makini, wakitumia vigezo vya kiisimu, kihistoria na kisaikolojia.

Maelezo ya kina kabisa ya uchambuzi wa aina hiyo hiyo yanapatikana katika maandishi ya Nurse na Hinnebusch (1993): Swahili and Sabaki: A Linguistic History, maandishi ambayo yamechapishwa kama Juzuu la 121 katika mfululizo wa jarida la Linguistics.

Ni muhimu pia kuwataja Shihabuddin Chiraghdin na Mathias Mnyapala, ambao katika kitabu chao cha ‘Historia ya Kiswahili’ (1977) na maandishi yao mengine juu ya historia na maendeleo ya lugha ya Kiswahili nao wametoa mchango mkubwa sana.

Kijumla, kuna mwoano mkubwa wa Kiswahili na lugha za Kibantu hasa katika masuala ya kifonetiki.

 

[email protected]