• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Watu waliojihami washambulia kijiji cha Kisii mjini Thika

Watu waliojihami washambulia kijiji cha Kisii mjini Thika

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Kisii mjini Thika, walipigwa na butwaa baada ya watu waliojihami kwa vifaa butu kuvamia makazi yao na kubomoa nyumba.

Wakazi wengi waliacha mali yao nyuma wakiogopa kujeruhiwa na wavamizi hao ambao hawakuwa na huruma na yeyote.

Uchunguzi uliofanywa unaeleza ya kwamba kampuni moja ya kuuza mashamba eneo za Thika Mashariki ndiyo inapanga kuwafurusha wakazi hao ambao walinunua vipande vya ardhi sehemu hizo na kujenga nyumba zao huko.

Mkazi wa kijiji hicho, Bi Susan Wakonyo anasema ilikuwa mwendo wa saa tano za usiku mnamo Jumamosi wakati wavamizi hao walivamia wakazi hao kwa kuwapiga bila huruma.

“Nilijenga nyumba ya vyumba viwili na ninaishi hapo na watoto wangu. Sasa ninashangaa kuona ya kwamba tunahamishwa kama wezi,” alisema Bi Wakonyo.

Inadaiwa kuwa wavamizi hao walikata nyaya za umeme ili wapate nafasi ya kuwafurusha wakazi hao kwenye giza.

Mwakilishi wa mbunge wa Thika Bw John Mwangi, alisema polisi wamezembea sana baada ya tukio hilo kutendeka.

“Tutafanya juhudi kuona ya kwamba tunawasiliana na Wizara ya Ardhi ili izuru eneo hilo na kutatua shida hiyo. Wakazi wengi hapo walinunua ardhi hiyo na kujenga nyumba zao hapo,” alisema Bw Mwangi.

Alisema ni vyema Wizara ya Ardhi ifike eneo hilo ili iweze kutanzua shida kubwa inayoshudiwa na wakazi hao.

Yasikitisha

Aliongeza kuwa wengi wao walinunua vipande vya ardhi hiyo kihalali lakini inasikitisha kuona wakifurushwa.

Alisema ya kwamba wiki moja iliyopita kulitokea migogoro ya ardhi kijiji cha Kiganjo ambapo jambo hilo linafuatiliwa na idara husika.

Mkazi mwingine John Kimani alisema nyumba yake ilibomolewa huku dirisha na milango ikivunjwa.

“Tunaiomba serikai kuingilia kati kuona ya kwamba wote waliohusika na kitendo hicho cha kinyama wanachukuliwa hatua ya haraka kwa sababu tumebaki pweke bila kujua la kufanya,” alisema Bw Kimani.

Hadi wakati wa kuchapishwa habari hii wakazi wengi wameachwa bila makao maalum baada ya wavamizi hao waliotumwa kutekeleza unyama huo.

Wanaiomba serikali kuingilia kati na kuwasaka ili wafunguliwe mashtaka.

Inadaiwa walikuwa wamejihami kwa majembe, marungu, mapanga na shoka huku lengo lao kuu likiwa ni kuvunja nyumba yoyote walioifikia.

Wakati huo kila mmoja alijaribu kujinusuru kwa kuondoka mbio bila kutazama nyuma.

  • Tags

You can share this post!

Mhubiri ajiua baada ya kumsababishia mke majeraha yaliyomuua

Shughuli za usafiri uwanja wa ndege wa Manda zarejelewa...

adminleo