Shughuli za usafiri uwanja wa ndege wa Manda zarejelewa kama kawaida
Na KALUME KAZUNGU
SHUGHULI za usafiri katika uwanja wa ndege wa Manda, Kaunti ya Lamu zimerejelewa kama kawaida baada ya uwanja huo wa ndege kufungwa kwa muda Jumapili kufuatia shambulio la al-Shabaab lililolenga kambi ya wanajeshi wanamaji na ile ya wanajeshi wa Amerika iliyoko karibu na uwanja huo wa ndege.
Wapiganaji watano wa kundi hilo waliuawa huku wengine watano wakikamatwa wakiwa hai wakati wa shambulio hilo la majira ya saa kumi na moja na nusu alfajiri.
Halmashauri ya usimamizi wa viwanja vya ndege na usafiri nchini (KCAA) ilitangaza kurejelewa kwa shughuli za usafiri uwanjani hapo muda wa saa chache baada ya kufungwa kufuatia shambulio lililokuwa limetokea Jumapili asubuhi.
“Halmashauri ya KCAA ingependa kuwatangazia wadau wote wa usafiri wa ndege na umma kwamba baada ya uvamizi wa kigaidi asubuhi, kufungwa kwa muda kwa uwanja wa ndege wa Manda kulikokuwa kumetangazwa awali sasa kumeondolewa kupisha shughuli za kawaida kuendelea,” ikasema KCAA katika ujumbe wake.
Akizungumza Jumatatu na ‘Taifa Leo’, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia amefafanua kwamba kufungwa kwa uwanja wa ndege wa Manda hakukutokana na kwamba uwanja huo ulikuwa umevamiwa bali ilikuwa tahadhari ya kiusalama.
Bw Macharia ameshikilia kuwa usalama umedhibitiwa vilivyo kwenye uwanja huo na kuwataka wafanyakazi na hata wasafiri wanaotumia uwanja huo kuondoa shaka.
“Shughuli zilisitishwa baada ya uvamizi wa kigaidi kutekelezwa kwenye kambi za wanamaji na ile ya Amerika eneo la Manda Bay na wala si ndani ya uwanja wa ndege wa Manda. Kwa sasa usalama umeimarishwa vilivyo na hakuna sababu ya watu kutishika,” akasema Bw Macharia.