• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
SHINA LA UHAI: Madhara ya ukeketaji kwa afya ya wanawake

SHINA LA UHAI: Madhara ya ukeketaji kwa afya ya wanawake

Na PAULINE ONGAJI

ALIPOKEKETWA akiwa msichana wa umri wa miaka 13 pekee wakati huo, wazazi wake Chemoyo Lopuonyang, walikuwa na uhakika kwamba binti yao angewaletea utajiri mwingi kutokana na mahari waliyohakikishiwa kutoka kwa waliotamani kumposa.

Lakini hata kabla ya kidonda chake kupona, tayari Bi Lopuonyang ambaye kwa sasa ni mwanamke wa miaka 40, alikumbana ana kwa ana na madhara yanayotokana na kupashwa tohara.

“Nilivuja damu kwa siku tatu mfululizo, suala lililonifanya nipelekwe hospitalini na kuongezewa damu,” aeleza mkazi huyu wa kijiji cha Kalpunyany, Kaunti ya Baringo.

Lakini masaibu yake hayakuishia hapo kwani madhara yanayotokana na ukeketaji yalimfuata hata katika ndoa. “Nilipokuwa naolewa, uke wangu ulikuwa umejifunga kidogo, suala lililowalazimu kunikata kwa kutumia upanga ili kufanya iwe rahisi kwa mume wangu kupenya wakati wa tendo la ndoa,” aeleza.

Kilichofuatia kilikuwa mimba iliyodumu kwa miezi sita pekee ambapo pacha wake wawili walizaliwa kabla ya muda wa ujauzito kukamilika, na wakafariki. Sio hayo tu, wakati wa kujifungua alikumbwa na nasuri ya uzazi, hali iliyoweka ndoa yake kwenye hatari.

Hata hivyo kwa bahati nzuri alipona na kurejea kwa mumewe ambapo baadaye alijifungua pacha wengine watatu. Lakini hii haikuwa bila masaibu kibao ya kiafya, suala lililomlazimu kupelekwa hospitali kila mara.

Kwa kawaida ukeketaji huhusisha kukata baadhi ya sehemu za kinembe au mdomo wa uke kwa sababu zisizo za kimatibabu.

Watu kutoka jamii zinazotekeleza utamaduni huu wanaamini kwamba hii ni njia ya kukata kiu ya mahaba miongoni mwa wanawake, na hivyo kuhakikisha kwamba wanadumisha maadili hasa baada ya kuolewa.

Hata hivyo, shughuli hii imeonekana kukiuka haki za wasichana na wanawake hasa kutokana na matatizo ya kiafya yanayowaandama wale ambao waliwahi kupashwa tohara.

Matatizo

Kulingana na Penina Titimo, mhudumu na naibu mratibu wa masuala ya afya ya uzazi katika Kaunti ya Pokot Magharibi, kuna matatizo kadha wa kadha yanayotokana na ukeketaji.

“Mwanzoni, mhusika ana uwezekano mkubwa wa kukumbwa na maumivu, kuvuja damu, pepopunda, matatizo ya kukojoa, vidonda na majeraha kwenye tishu za sehemu ya uzazi. Kwa upande mwingine, kuna madhara ya baadaye kama vile kukumbwa na maambukizi kwenye mfumo wa mkojo, utasa, matatizo wakati wa kujifungua kila mara,” aeleza.

Utafiti uliofanywa katika wilaya nne nchini na chama cha Maendeleo ya Wanawake mwaka wa 1993 ulionyesha kwamba asilimia 48.5 ya wanawake waliokeketwa walivuja damu huku asilimia 23.9 wakikumbwa na maambukizi na asilimia 19.4 wakipata matatizo ya kukojoa baada ya kukeketwa.

Kuhusiana na matatizo wakati wa kujifungua, Shirika la Afya Duniani-WHO laonyesha kwamba, wanawake ambao wamekeketwa wana uwezekano mkubwa wa kukumbwa na matatizo wakati wa kujifungua.

Kwa mfano, visa vingi vya kujifungua kupitia upasuaji, vile vile kuvuja damu wakati wa kujifungua vilionekana kuwakumba wanawake wengi waliopashwa tohara, wakilinganishwa na wenzao ambao hawajakeketwa.

Aidha, utafiti uliofanywa mwaka wa 2008 na WHO ulionyesha kwamba visa vingi vya vifo vya watoto na akina mama wakati wa kujifungua viliripotiwa miongoni mwa wanawake waliopashwa tohara.

Lakini licha ya uhalisia huu wa kutisha, bado imekuwa vigumu kushawishi jamii hizi kuhusu hatari zinazotokana na desturi hii.

Mwaka wa 2011, Kenya ilipitisha sheria iliyopiga marufuku ukeketaji nchini kote, ambapo ni hatia kutekeleza ukeketaji au kumpeleka mtu nchi nyingine ili kukeketwa.

Ni suala ambalo limekuwa na matokeo mema kwa kiwango fulani. Kwa mfano, kulingana na Kamishna wa Kaunti ya Pokot Magharibi, Okello Apolo, kuna upungufu wa visa vya ukeketaji eneo la Pokot Magharibi, suala linalojiakisi kutokana na kupungua kwa idadi ya wasichana wanaoacha shule ili kuolewa.

“Tumeshuhudia asilimia 86 ya wanafunzi kutoka shule ya msingi wanaojiunga na shule za upili. Mwaka wa 2019, zaidi ya wanafunzi 140,000 walifanya mtihani wa kitaifa wa KCPE na tunatarajia wengi wajiunge na shule za upili,” asema.

Hata hivyo, bado utamaduni huu unazidi kutekelezwa kisiri katika sehemu tofauti nchini. huku baadhi ya watu wakibuni mbinu za kutekeleza uhalifu huu kisiri.

Kulingana na Bw Okello, baadhi ya wazazi wa kisasa ambao bado wanashikilia utamaduni huu wameamua kusaka huduma za wahudumu wa kiafya. “Kumekuwa na fununu za visa vya wasichana kukeketwa na wahudumu wa kiafya katika vituo vya kimatibabu. Wengi wanafanya hivi kisiri kama mbinu ya kujiepusha na mkono wa sheria,” aeleza.

James Lokuk, mwalimu mkuu wa Morpus Rescue Center; shule ya msingi ambayo pia ni makao ya wasichana waliotoroka ukeketaji na ndoa za mapema eneo la Pokot Magharibi, aidha anasema kwamba siku hizi watu wamebuni mbinu mpya za kutekeleza ukeketaji.

“Hapa, msichana anapelekwa kwa mumewe na mahari kutolewa kabla ya yeye kukeketwa. Anatarajiwa kukaa huko hadi atakapotimu umri wa kuolewa ambapo atakeketwa na kuolewa rasmi,” aeleza.

Jessica(Sio jina lake halisi) ni mmoja wa wasichana waliopangiwa kuozwa kupitia njia hii lakini kwa bahati nzuri akatoweka kabla ya kutimiza hayo. Msichana huyu wa miaka 13, ni mmojawapo wa wasichana wachanga katika kituo cha Morpus Rescue Center.

Hadithi yake ni ya ukakamavu hasa ikizingatiwa kwamba alilazimika kukimbia kilomita kadha kutoka kwa boma ambapo alikuwa ameozwa kwa kibabu. “Wazazi wangu walikuwa wamenioza kwa mwanamume huyu na walikuwa wanapanga nitahiriwe kabla ya kuwa mkewe rasmi,” asema.

Lakini ni mtego ambao mwanafunzi huyu wa darasa la sita alifanikiwa kukwepa ila bado anaishi kwa hofu kuwa jamaa zake watakuja kumchukua na kumuoza tena.

Bi Lopuonyang anasema kwamba tatizo sio tu miongoni mwa wanaotekeleza utamaduni huu uliopigwa marufuku, bali pia wanaoathirika kutokana na utamaduni huu.

“Kulingana na utamaduni wa watu wa jamii ya Pokot, mwanamke ambaye hajakeketwa anachukuliwa kuwa mtoto mdogo na hakuna anayetaka kumuoa. Na hata akiolewa, kejeli anazopokea humsukuma yeye mwenyewe kwenda kusaka huduma za wakeketaji,” aongeza Lopuonyang.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kenya Health and Demographic Survey 2014, idadi ya wanawake waliokeketwa huongezeka kuambatana na umri huku wanawake wa Kiislamu wakiwa katika uwezekano mkubwa wa kukeketwa (asilimia 51) wakilinganishwa na wenzao kutoka dini zingine.

Ripoti hii aidha inafichua kwamba wanawake wa Kiisilamu wana uwezekano mkubwa wa kuwahi kufanyiwa ukeketaji unaohusisha kushonwa na kuzibwa uke (asilimia 30) wakilinganishwa na wanawake wa dini zingine (kati ya asilimia 4 na 6).

Aidha, idadi ya wanawake waliokeketwa nchini hutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine huku wanawake kutoka jamii ya Somali wakiongoza kwa asilimia 94. Jamii ya Samburu kulingana na ripoti hiyo ni ya pili kwa idadi ya wanawake wanaotahiriwa wakiwakilisha asilimia 86.

Jamii ya Kisii ni ya tatu ikisimama kwa asilimia 84 na Wamaasai wakifunga nafasi nne za mwanzo kwa asilimia 78. Kwa upande mwingine idadi ya wanawake wanaopashwa tohara miongoni mwa jamii za Waluo, Waluhya, Turkana na Mijikenda/Swahili iko chini ya asilimia 2.

John Wafula, mtaalamu wa masuala ya uhisani katika Hazina ya Umoja wa Mataifa inayohusika na idadi ya watu-UNFPA anasema kwamba japo visa vya ukeketaji vilipungua kutoka asilimia 27 mwaka wa 2008 hadi asilimia 21 mwaka wa 2009 kulingana na ripoti ya 2014 Kenya Demographic and Health Survey (2014 KDHS), bado mengi yanahitajika kufanywa ili kuangamiza utamaduni huu.

“Suluhu inapaswa kumkumbatia kila mmoja badala ya kutumia nguvu. Kuna haja ya kufanya jamii hizi kuelewa madhara yanayotokana na ukeketaji. Hii inahitaji harakati za kuelimisha jamii hizi kushika kasi katika viwango vya kitaifa,” aongeza.

You can share this post!

Sonko ateua naibu, MCA wakijadili hatima yake

SURA TISHO: Liverpool yaicharaza Everton 1-0 dimba la FA

adminleo