Mvua ya mauti watu 22 wakiangamia
Na WAANDISHI WETU
ZAIDI ya watu 22 walifariki dunia Jumanne kwenye mikasa miwili tofauti inayohusiana na mvua, huku idara ya utabiri wa hali ya hewa ikionya kuwa, mvua kubwa inatarajiwa leo katika maeneo kadhaa nchini.
Kwenye mkasa wa kwanza, tukienda mitamboni polisi walikuwa wamethibitisha vifo vya watu 19 ambao basi walilokuwa wakisafiria lilipoteza mwelekeo na kutumbukia kwenye mto katika barabara ya Narok-Maai Mahiu.
Basi hilo linalobeba abiria 62 la kampuni ya Daima Connection Sacco lilikuwa likisafiri kuelekea Nairobi kutoka Kendu Bay lilipotumbukia ndani ya Mto Siyiapei jana saa tisa na dakika 30 alasiri.
Kamishna wa Kaunti ya Narok, Bw George Natembeya alisema abiria wawili walikuwa mahututi na wengine 42 walitibiwa katika hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Narok wakiwa na majeraha madogo.
Alieleza kuwa basi hilo lilikuwa likiendeshwa kwa kasi, ilhali kulikuwa kumekesha mvua kubwa usiku kucha.
“Basi lilikuwa lilijaribu kupita lori mita chache kutoka kwa daraja, kabla ya kugonga vyuma vya reli kwa upande mmoja wa daraja na kutumbukia mtoni,” alisema Bw Natembeya.
Miongoni mwa waliofariki ni watu wazima 16 na mtoto. Ajali hiyo iliibua kumbukumbu za ajali nyingine iliyotokea Agosti 2013 ambapo watu 41 walifariki na 44 kujeruhiwa, basi kutoka Homa Bay lilipobingiria mara kadha katika eneo la Ntulele, Narok.
Kwingineko, katika kaunti ya Tana River watu watatu waliuawa na mafuriko katika eneo la Bura, baada ya mvua kunyesha kwa zaidi ya saa 15.
Watoto
Watoto wawili wa umri wa miaka mitatu na mwingine wa miaka mitano walipatikana wakielea katika kidimbwi cha maji taka nyuma ya nyumba yao, huku mama mmoja akitolewa katika maji ya kivuko cha kuingia Bura.
OCPD wa eneo la Bura, Bw Tom Okoth, alielezea Taifa Leo kwamba, miili ya watoto hao ilionekana na mpita njia aliyewaarifu polisi baada ya kuwatoa katika kidimbwi hicho, huku wakazi wakiwajulisha askari kuhusu mwili wa mwanamke katika kivuko cha Bura.
Na jijini Nairobi, Mkurugenzi wa idara ya hali ya hewa, Bw Peter Ambenje alisema mvua kubwa inatarajiwa maeneo ya nyanda za juu ya Kati ambayo ni pamoja na Nairobi, Magharibi, Kusini mwa Rift Valley, Kaskazini Mashariki na Kusini mashariki kuanzia Jumatano hadi Ijumaa asubuhi.
Pia alisema Pwani Kusini kunatarajiwa mvua kubwa Ijumaa. Kwa sasa, maeneo kadha nchini hasa Pwani, sehemu za Mashariki na Kaskazini Mashariki zinapokea mvua kubwa ambayo imesababisha mafuriko.
“Sehemu kadha nchini zinatarajiwa kuendelea kupokea mvua kwa siku saba zijazo huku mvua kubwa ikitarajiwa nyanda za juu ya Kati ambayo ni pamoja na Nairobi, Magharibi, Kusini mwa Rift Valley, Kaskazini Mashariki na Kusini mashariki kuanzia Jumanne jioni hadi Ijumaa asubuhi,” alisema Bw Ambenje.
Alieleza kuwa siku saba zilizopita, kiasi cha mvua kimeongezeka katika maeneo kadha nchini kituo cha Kitui kikirekodi kiasi cha juu zaidi cha milimita 254.1, ambayo inatambuliwa kuwa mvua kubwa.