Wafanyakazi 2,000 mradi wa Lapsset watumwa nyumbani, waambiwa wasubiri neno la mwajiri
Na KALUME KAZUNGU
WAFANYAKAZI zaidi ya 2,000 wanaoendeleza ujenzi wa mradi wa Bandari Mpya ya Lamu (Lapsset) wametumwa nyumbani ghafla baada ya mkandarasi wa mradi huo kuhofia huenda wafanyakazi hao wakalengwa na kushambuliwa na wapiganaji wa al-Shabaab.
Hii ni kufuatia tukio la kigaidi mnamo Jumapili ambapo al-Shabaab walivamia kambi ya wanajeshi wa majini (nevi) na ile ya wanajeshi wa Amerika zilizoko eneo la Manda-Magogoni, Kaunti ya Lamu.
Eneo la Kililana ambako Lapsset inajengwa ni umbali wa kilomita moja pekee kutoka kambi hiyo iliyoshambuliwa ya Manda-Magogoni.
Kupitia tangazo rasmi ambalo ‘Taifa Leo’ imeona, kampuni iliyopewa kandarasi ya ujenzi wa Lapsset ya China Communications Construction Company (CCCC), imewafahamisha wafanyakazi wake wote kwamba shughuli za ujenzi eneo hilo zimesitishwa kwa muda na kwamba vibarua wote wanatakiwa kurudi nyumbani.
“Kambi ya jeshi la wanamaji eneo la Manda-Magogoni ilishambulia na al-Shabaab Januari 5, 2020, na kufuatia hali ya usalama wa Lamu ambayo bado si nzuri, tumeafikia kufunga shughuli zote za kikazi hapa Lapsset hadi Januari 13 ambapo mtajulishwa iwapo tutafungua tena shughuli hapa. Tunawasihi wafanyakazi wote kurudi nyumbani,” linasema tangazo hilo.
Akithibitisha kufungwa kwa shughuli za kikazi kwenye bandari ya Lamu, Meneja wa Lapsset, tawi la Lamu, Salim Bunu, amesema tayari wameanzisha mazungumzo na mwanakadnarasi ili shughuli zirejelewe hivi karibuni.
“Ni kweli. Shughuli za ujenzi wa LAPSSET zimesitishwa na tayari mwanakandarasi amewatuma wafanyakazi wote nyumbani hadi Januari 13 ambapo watatangaziwa tena kurudi. Hata hivyo tunaandaa mazungumzo na mwanakandarasi ambaye ni CCCC ili kuona kwamba ujenzi wa Lapsset unarejelewa kama kawaida wakati wowote kuanzia sasa,” akasema Bw Bunu.
Afisa wa Halmashauri ya Bandari (KPA), tawi la Lamu, Abdishukri Osman pia amethibitisha kufungwa kwa shughuli za ujenzi eneo la Lapsset.
Bw Osman alisema majadiliano yanaendelea kati ya mwanakandarasi, KPA, idara ya usalama na Lapsset kwa jumla ili kuona kwamba shughuli zinarejelewa mara moja.
“Tunaelewa wasiwasi wa mkandarasi kwamba hataki wafanyakazi wake wadhuriwe na al-Shabaab. Hata hivyo idara ya usalama tayari imetuhakikishia usalama wa kutosha. Hata wanajeshi wa Kenya (KDF) wametumwa kulinda eneo la Lapsset. Tutajadiliana na wadau ili kuona kwamba shughuli zinarejelewa mara moja eneo hilo la Lapsset,” akasema Bw Osman.
Tangu magaidi wa Al-Shabaab kuvamia kambi ya nevi huko Lamu, wakazi hasa wa vijiji vinavyokaribiana na kambi hiyo, ikiwemo Magogoni, Mkondoni, Kwasasi, Sina Mbio, Kauthara na maeneo yaliyokaribiana wamekuwa wakiishi kwa taharuki.
Uchunguzi uliofanywa na ‘Taifa Leo’ juma hili ulibaini kwamba wakazi wengi wa vijiji husika tayari wameanza kuhama makwao na kukimbilia mjini Hindi kwa kuhofia usalama wao.
Kufikia Jumanne, familia zipatazo 50 tayari zilikuwa zimehama kwenye vijiji vyao na kutafuta makao salama mjini Hindi.
Katika kijiji cha Mkondoni, Mzee wa kijiji hicho, Hassan Chonde ameambia ‘Taifa Leo’ kwamba kati ya familia 86 zinazoishi eneo hilo, ni familia 20 pekee ambazo zimebakia ilhali wengine wakitorokea Hindi.
Bw Chonde amesema baadhi ya wakazi wamelazimika kulala msituni kila jioni kwa kuhofia kulengwa na kuuawa na al-Shabaab.
“Hapa Mkondoni kuna zaidi ya familia 86 lakini kufikia sasa ni familia 20 pekee zilizobaki. Wengi wamehamia mjini Hindi kwa hofu kwamba huenda Al-Shabaab wakawalenga na kuwaua,” akasema Bw Chonde.
Katika kijiji cha Sina Mbio kati ya familia 50 zinazoishi eneo hilo, ni familia 10 pekee ndizo ambazo kufikia Jumanne zilikuwa hazijaondoka kwenye makazi yao ambapo familia nyingi tayari zimetorokea mjini Hindi.
‘Taifa Leo’ pia imeshuhudia wakazi wakibeba vitanda, magodogo na hata mifugo, wengine wakitembea kwa miguu ilhali wengine wakibeba vyombo vyao kwa pikipiki kuelekea eneo salama la Hindi.
Mkazi wa Kauthara, Bi Maria Kimani amesema kuna haja ya serikali kuimarisha zaidi usalama kwenye vijiji vyao ili wakazi waishi bila hofu.
“Tuko na wasiwasi tangu tuliposikia Al-Shabaab wamevamia kambi ya jeshi eneo la Manda-Magogoni na pia eneo la Nyongoro kwenye barabara kuu ya Lamu kuelekea Mombasa. Tunajiuliza, ikiwa hao magaidi wanaweza kuvamia kambi ya jeshi, je sisi raia tufanyeje. Tuko na uoga mwingi na ndio sababu tunahama vijijini mwetu. Serikali itupe hakikisho katika suala hili la usalama,” akasema Bi Kimani.
Katika kijiji cha Magogoni, takriban familia zote zinazoishi eneo hilo zilikuwa zimehama makwao kwa kuhofia kushambuliwa na Al-Shabaab.
Mkazi wa Magogoni Bw Paul Mwaura amesema kijiji chao ndicho kinachopakana kabisa na kambi ya jeshi iliyovamiwa ya Manda-Magogoni.
“Inamaanisha wakitoka kwenye kambi ya jeshi wataingia vijijini mwetu kutumaliza hawa magaidi. Siwezi kuendelea kuishi hapa. Heri nihame hadi pale serikali itakapotuliza kadhia ya al-Shabaab,” akasema Bw Mwaura.
Katika kikao na wanahabari Jumanne, Idara ya Usalama, Kaunti ya Lamu, ikiongozwa na Kamishna wa eneo hilo, Irungu Macharia na Kamanda wa Polisi eneo hilo, Muchangi Kioi, imewahakikishia wakazi usalama wa kutosha na kuwataka kutohama vijijini.
“Tumedhibiti usalama vilivyo kote Lamu na sioni haja ya watu kubabaika na hata wengine kuhama. Maafisa wa usalama wamesambazwa kila mahali. Cha msingi ni nyinyi wakazi kuishi kwa amani na kuendelea na shughuli zenu kama kawaida,” amesema Bw Macharia.