• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 12:32 PM
56 wafa katika mkanyagano Qasem Soleimani akizikwa

56 wafa katika mkanyagano Qasem Soleimani akizikwa

Na MASHIRIKA

WATU 56 walifariki Jumanne katika mkanyagano uliotokea wakati wa mazishi ya Luteni Jenerali Qasem Soleiman aliyeuawa na majeshi ya Amerika nchini Iraq Ijumaa iliyopita.

Watu wengine 200 walijeruhiwa wakati wa mazishi hayo ambayo yalihudhuriwa na maelfu ya waombolezaji.

Mamia ya maelfu ya waombolezaji walianza kumiminika mjini humo Jumatatu jioni kuhudhuria mazishi hayo ya Soleimani aliyekuwa kiongozi wa kikosi cha Iran kwa jina Quds Force. Aliuawa karibu na uwanja wa kimataifa wa ndege jijini Baghdad, Iraq kwa amri ya kijeshi iliyotolewa na Rais wa Amerika Donald Trump.

Awali, video iliyopakiwa mitandaoni iliyonyesha miili ya watu ikiwa imetapakaa katika barabara moja huku watu wengine wakipiga kelele na kujaribu kuwasaidia

Pirhossein Koulivand, ambaye ni mkuu wa shirika la kutoa matibabu ya dharura nchini Iran, alihojiwa na runinga ya kitaifa na akathibitisha kuwa kulitokea mkanyagano wa watu.

“Kwa bahati mbaya kufuatia mkanyagano huo, baadhi ya watu wamejeruhiwa na wengine wamefariki wakati wa msafara wa mazishi,” akasema.

Mnamo Jumatano, msafara wa kumuenzi jijini Tehran ulivutia zaidi ya watu milioni moja, waliosongamana katika baadhi ya barabara kuu na zile ndogo.

Kiongozi wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei aliangua kilio hadharani alipoongoza maombi ya kumuaga mwendazake katika uwanja ulioko nje ya Chuo Kikuu cha Tehran.

Mazishi ya Jumanne yalifanyika baada ya misafara kufanyika kwa siku kadhaa na iliyoanza katika barabara za mji wa Ahvaz iliyoko kusini mwa Iran. Misafara mingine pia ilifanyika katika mji wa Mashhad ulioko Kaskazini Magharibi mwa Iran, Jiji takatifu la Qom na hatimaye jiji kuu Tehran.

Huzuni iliyotanda nchini humo ilitajwa kama ya kipekee kwa heshima ya kiongozi huyo wa kijeshi aliyesawiriwa kama shujaa nchini humo kutokana uongozi wake wa kikosi cha Quds Force.

Soleimani, alifariki akiwa na umri wa miaka 62, aliongoza operesheni ya wanajeshi wa Irani katika ukanda wa mashariki ya kati, kiasi cha kuchukuliwa na Amerika kama gaidi sugu.

Kwa mujibu wa Rais Trump, aliamuru Soleimani auawe kwa sababu alikuwa akipanga kufanya mashambulio makali katika ubalozi na kambi ya wanajeshi wa Amerika nchini Iraq na mataifa mengine katika eneo la Mashariki ya Kati.

Iran imetangaza kuwa italipiza kisasi mauaji ya kiongozi huyo wa kijeshi huku bunge la nchi hiyo jana likipitisha hoja ya kuwachukulia wanajeshi wa Amerika kama “magaidi”.

You can share this post!

MAPISHI: Jinsi ya kuandaa wali wa nazi na nyama ya kusaga

KINA CHA FIKIRA: Taaluma ya Kiswahili yahitaji asasi...

adminleo