Habari

Tangatanga wakubali Uhuru awe Waziri Mkuu

January 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

ERIC MATARA na NICHOLAS KOMU

VIONGOZI wa kisiasa kutoka eneo la Rift Valley wamesema wanaunga mkono wazo la Rais Uhuru Kenyatta kuwa Waziri Mkuu 2022, ikiwa Naibu Rais William Ruto ndiye atakayekuwa Rais.

Matamshi hayo yalitolewa huku Dkt Ruto kwa upande wake akitangaza kwamba ana Uhakika Rais Kenyatta hana nia ya kuongeza kipindi chake cha uongozi wa nchi baada ya 2022.

Ijapokuwa Rais huepuka kutangaza msimamo wake kuhusu suala hilo, amewahi kusema akiwa Kaunti ya Nyeri kwamba hatajali ikiamuliwa aendelee kuwa uongozini.

Wanasiasa hao wa kikundi cha Tangatanga waliojumuisha Nelson Koech (Belgut), Joseph Tonui (Kuresoi) na David Sankok (Mbunge Maalum), walikubaliana na viongozi wengine wanaosema Rais Kenyatta angali kijana na anayeweza kuendelea kutumikia nchi.

Bw Koech alisema: “Ikiwa Rais Kenyatta anahisi kuwa bado ana nguvu na amejitolea kwa ajenda ya Jubilee, basi ni sawa kwake kuwa Waziri Mkuu na Dkt Ruto kuwa Rais. Itakuwa sawa kwa vyeo hivi kusalia ndani ya chama cha Jubilee.”

Kulingana naye, hatua hii itatimiza maelewano kati ya wawili hao kwamba kila mmoja ataongoza kwa miaka 10.

“Wadhifa ambao Rais hawezi kuwania ni urais pekee kwa sababu Katiba ya sasa haimruhusu kufanya hivyo,” akafafanua Bw Koech.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Bw Sankok ambaye alikariri kuwa wawili hao wangali marafiki kinyume na inavyodhaniwa na wengi.

“Hakuna makosa kwa Rais Kenyatta kuwa Waziri Mkuu na Dkt Ruto kuwa Rais kwa sababu viongozi hawa wawili bado wana uhusiano mzuri,” Bw Sankok akasema Jumanne.

Bw Sankok alisema kuwa miradi mingi ya Jubilee ambayo inahitaji kukamilishwa inahitaji ushirikiano wa Rais Kenyatta na Dkt Ruto katika serikali ijayo.

Naye Bw Tonui aliwataka wafuasi wa Jubilee kupuuzilia mbali uvumi aliodai unaenezwa na wanasiasa wa upinzani kwamba kuna uadui kati ya Rais Kenyatta na naibu wake.

“Urafiki kati ya wawili hawa ulioanza 2013 waliposhtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) ungali imara. Kwa hivyo, sisi kama viongozi wa Rift Valley tunawataka waendelee kufanya kazi pamoja katika serikali ijayo,” akasema.

Lakini akizungumza Jumanne akiwa Nyeri, Dkt Ruto alisema: “Sidhani kama Rais ana mpango wowote wa kubadili Katiba ili kuongeza muda wake wa kuhudumu. Ninasema hivi kwa vile ninamjua vyema na anaheshimu demokrasia.”

Dkt Ruto alisema Rais tayari amefanikisha mengi yatakayomwashia sifa akiondoka mamlakani 2022 ikiwemo kuleta umoja wa taifa.

Wabunge Kuria Kimani (Molo) na Martha Wangari (Gilgil) walishikilia kuwa Rais Kenyatta anapaswa kustaafu kwa heshima.

“Rais mwenyewe amesema mara kadha kwamba anataka kustaafu. Sioni kwa nini baadhi ya viongozi bado wanataka aendelee kuwa uongozini,” akasema Bi Wangari.

Naye Bw Kimani alisema kusalia mamlakani kwa Rais Kenyatta kutamweka pamoja na viongozi wengine wa Afrika ambao wamekuwa wakikatalia mamlakani hata baada ya kipindi chao cha uongozi kukamilika.

Kauli hiyo za wabunge wa Jubilee zinafuatia pendekezo la aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe kwamba Rais Kenyatta atasalia mamlakani kupitia wadhifa wa Waziri Mkuu baada ya muhula wake wa pili kukamilika 2022.

Baadhi ya viongozi wanaoegemea mrengo wa kiongozi wa ODM Raila Odinga, akiwemo Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli, wameunga mkono kauli ya Bw Murathe.