Washukiwa wanne wa uhalifu wauawa Eldoret
Na TITUS OMINDE
MAAFISA wa polisi mjini Eldoret wamewapiga risasi na kuwaua watu wanne ambao walishukiwa kuwa wahalifu waliokuwa wamejihami.
Washukiwa hao, wamekuwa a polisi kwa siku tano zilizopita kabla ya kuuwawa kwa bunduki.
Maafisa wamesema watuhumiwa hao walikuwa katika gari dogo na walikataa kusimama waliposimamishwa na maafisa wa polisi waliokuwa kazini mjini humo katika barabara kuu ya Eldoret-Webuye, karibu na mtaa wa Posta.
Washukiwa hao, inadaiwa, kwamba walikuwa wanachama wa genge la majambazi wanaohusika na uhalifu jijini Nairobi, Nakuru, Eldoret miongoni mwa miji mingine mikubwa.
Akithibitisha tukio hilo Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Uasin-Gishu Bw Johnstone Ipara amesema maafisa hao walijibu kwa risasi wakiwalenga watuhumiwa baada ya kukataa kusimama.
Bw Ipara amesema watuhumiwa walikufa papo hapo baada ya gari walilokuwa wakitumia kumiminiwa risasi wakati wa tukio la saa mbili asubuhi.
Afisa huyo amesema watuhumiwa hao walikuwa wakipanga kujihusisha na vitendo vya uhalifu mjini humo kabla ya polisi kugundua mipango yao na kuwawekea mtego.
“Leo majira ya saa mbili asubuhi maafisa wetu ambao walikuwa kwenye doria walisimamisha gari ambalo lilikuwa likiendeshwa kwa njia hatari na watuhumiwa. Wakati maafisa wetu walijaribu kuwazuia walikataa na hapo ndipo walianza kuwapiga risasi,” amesema Bw Ipara
Washukiwa hao walipatikana na bastola moja iliyotengenezwa kutoka Brazil, risasi 11 za risasi, mtoto wa bunduki na simu moja ya rununu inayoshukiwa kutumika katika uhalifu.
Washukiwa hao pia wanaaminika kuwa miongoni mwa wahalifu waliowashambulia maafisa wa polisi wa Utawala mwaka 2019.