• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:03 AM
RIZIKI: Uuzaji wa ‘long’i’ za jinsia ya kike umemtia tabasamu

RIZIKI: Uuzaji wa ‘long’i’ za jinsia ya kike umemtia tabasamu

Na SAMMY WAWERU

ALIPOHAMIA Kaunti ya Nairobi, shabaha yake ilikuwa kujiimarisha kimapato na kimaisha.

Bw Simon Wa Wangare alikuwa akifanya vibarua vya hapa na pale eneo la Nyandarua.

“Wakati mwingine vingepatikana na mwingine vinakosa. Nilihamia Nairobi mwaka 2012,” anafichua Simon.

Kilichomkaribisha, ulikuwa uchuuzi wa bidhaa za kula na kunywa kama vile biskuti, mahamri na vinywaji kama soda.

Alikuwa na bahati kama mtende kwani alipata kibanda cha shughuli hiyo eneo la Githurai, mtaa ulioko kungani mwa jiji la Nairobi.

Ilimgharimu mtaji wa Sh30,000 pekee kuwekeza katika biashara hiyo.

“Kaka yangu alikuwa akiuza nguo na alinitafutia nafasi nikaingilia biashara,” anaelezea Simon ambaye ni baba wa watoto wawili sasa.

Gange hiyo ilimuitikia na kushika kasi kiasi cha kumuwezesha kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo miaka kadhaa baadaye, kama vile kununua ploti eneo la Mai Mahiu, na kuanza shughuli za ujenzi.

“Kwa sasa niko katika harakati za kukamilisha kujenga nyumba ya vyumba kadhaa. Nitaikodisha hivi karibuni,” anasema.

Anaiambia Taifa Leo kwamba 2018 alipanua mawazo na kuingilia uuzaji wa nguo za kike, mavazi anayosema yana mapato kuliko bidhaa za kula. Simon anasema alishawishiwa na nduguye pamoja na wafanyabiashara wanaouza mavazi ya kike.

“Anauza sketi zinazovaliwa na wanawake, hasa ofisini, ambazo soko lake ni mithili ya mahamri moto,” anadokeza.

Hata hivyo, Simon anauza suruali ndefu za kike, maarufu kama ‘long’i’. Ni za kipekee, ambazo wanawake huzitambua kama ‘tights’. Pia ana suruali fupi, yaani kaptura.

Suruali ndefu za jinsia ya kike. Picha/ Sammy Waweru

“Nilianza kwa mtaji wa Sh5,000 pekee,” anasema, akisisitiza ni hatua asiyojutia kamwe. Bei ya bidhaa zake ni kati ya Sh100 – 300 na kulingana na mjasirimali huyo hununua mavazi hayo kutoka soko maarufu la Gikomba lililoko jijini Nairobi.

Soko la Gikomba ni tajika nchini kwa nguo za bei nafuu, ambalo wafanyabiashara kutoka kona mbalimbali za nchi huendea bidhaa humo.

Aidha, limesaidia pakubwa katika sekta ya juakali ambayo inakadiriwa kuchangia zaidi ya asilimia 75 ya nguvukazi nchini.

Kwa kawaida siku yake huanza kwa kuwahi sokoni asubuhi na mapema ili kuwahi long’i bora.

Hata hivyo, anasema ameweza kuimarisha uhusiano kati yake na wafanyabiashara wanaouza kiujumla.

“Hunipigia simu kuniiitia bidhaa zinapoingia,” anaelezea.

Kulingana na mfanyabiashara John Maina, ambaye huuza blauzi ili kupata nguo bora, muuzaji hana budi ila kuamkia soko alfajiri na mapema.

Isitoshe, anahimiza haja ya kuimarisha uhusiano kati ya mfanyabiashara wa rejareja na wale wa kijumla, kauli inayowiana na ya Simon Wa Wangare.

“Wateja wanahitaji bidhaa bora na za kipekee,” anasema Bw Maina ambaye ana uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika uuzaji wa blauzi eneo la Githurai na Ruiru.

Wafanyabiashara hao wanasifia sekta ya juakali, hasa uuzaji wa nguo wakisema imesaidia kubuni nafasi za ajira miongoni mwa vijana.

Mwaka 2017, baada ya kuchaguliwa kuhudumu awamu ya pili na ya mwisho, Rais Uhuru Kenyatta aliahidi kustawisha sekta ya juakali, ahadi ambazo zinaonekana kuwa hewa tu.

Mazingira ya wafanyabiashara wadogo na wale kadri, almaarufu SMEs, yangali duni, wachuuzi wa maeneo ya mijini wakilalamikia kuhangaishwa na askari wa halmashauri ya jiji, kanju. Mapema mwaka huu, 2020, serikali ilitangaza kuanza kutoza ushuru wa asilimia 3 kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kila mwaka.

Kulingana na Michael Muriuki, mjuzi wa masuala ya kiuchumi na biashara, hatua hiyo ni ya kukandamiza wafanyabiashara kama kina Simon na Maina.

“Kuna ada wanayolipia kila siku au mwezi. Kuwatoza ushuru mwingine ni ishara ya kuwahangaisha. Kutaja kuimarisha mazingira ya SMEs, Rais aangazie masuala kama hayo,” anahimiza Bw Muriuki.

Wakati wa mahojiano, Bw Simon alisema kila siku hulipa maafisa wa kaunti wanaokusanya ushuru ambapo ada anasema ni Sh20.

“Huja kuchukua kila siku,” akasema, akionekana kushangazwa na serikali kuanza kutoza ushuru wa asilimia tatu kila mwaka.

Licha ya pandashuka hizo, mfanyabiashara huyo anasema anapania kufungua kibanda kingine eneo la Progressive.

“Hivi karibuni nitapanua hii kazi. Tunachoomba, serikali iyafanye mazingira kuwa bora na salama kwa wafanyabiashara wadogo wadogo,” anarai.

Amebuni nafasi ya kijana mmoja, ambaye humsaidia kuuza, hasa anapoamkia soko na wakati amebanwa na shughuli za kibinafsi.

You can share this post!

Mahakama yaamuru serikali ijibu kesi ya Miguna

Miguna anavyojikaanga mwenyewe

adminleo