• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Kisasi dhidi ya Amerika ni lazima – Iran

Kisasi dhidi ya Amerika ni lazima – Iran

NA AFP

TEHRAN, IRAN

MAZISHI ya Luteni Jenerali Qasem Soleimani, ambaye aliuawa kutokana na shambulizi la majeshi ya Marekani nchini Iraq mnamo Ijumaa iliyopita, yanatarajiwa kufanyika leo katika mji wa Kerman, Iran.

Maelfu ya waombolezaji jana walimiminika katika barabara za mji wa Tehran kushuhudia msafara wa mwisho wa Soleimani, ambaye aliuawa kwa amri ya kijeshi iliyotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump.

Kiongozi wa Kidini wa Iran, Ayatollah Khamenei aliongoza maombi ya kumuaga mwendazake jijini humo na kwa wakati mmoja alionekana akidondokwa na machozi baada ya kuzidiwa na hisia za kupoteza mwanajeshi aliyeheshimika sana nchini humo.

Iran tayari imetangaza kwamba italipiza kisasi mauaji ya mwanajeshi huyo huku pia ikijiondoa kwenye maafikiano ya mwaka wa 2015 ya kudhibiti uundaji wa zana za kinuklia.

Soleimani, aliyekuwa na umri wa miaka 62, aliongoza oparesheni ya kijeshi ya Iran katika ukanda wa Mashariki ya Kati na alichukuliwa kama gaidi sugu na Marekani.

Kwa mujibu wa Rais Trump, Soleimani alikuwa akipanga kufanya mashambulizi makali kwenye ubalozi na kambi ya wanajeshi wa Marekani nchini Iraq na mataifa mengine ya Mashariki ya Kati.

Msafara huo wa kumuenzi ulipeperushwa moja kwa moja kwenye runinga ya serikali iliyoonyesha maelfu ya raia wakimiminika barabarani kumpa mwendazake waliyemtaja kama shujaa, heshima zake za mwisho.

Raia walionekana wakipiga nduru hadharani wengine wakiamua kunasa picha za msafara uliokuwa umebeba mwili wa marehemu, huku wakiimba nyimbo za kukashifu Marekani na kushinikiza serikali yao ilipize kisasi.

Bintiye marehemu, Zeinab Soleimani naye alionya Marekani itarajie siku za giza hapo mbeleni, akiahidi kwamba kifo cha babake lazima kilipiziwe kisasi.

“Mwendawazimu Trump, usifikirie kwamba kila kitu kimekamilika kufuatia mauaji ya kinyama ya babangu,” akasema Zeinab.

Rais wa Iran, Hassan Rouhani, ambaye alitembelea familia za mwanajeshi huyo, alisema Marekani itajuta kwa mauaji ya mwanajeshi huyo.

“Kisasi kutokana na kifo chake kitalipizwa siku ambayo unyama wa Marekani utakomeshwa kabisa katika mataifa ya Kiarabu,”; akasema Rais huyo.

Wikendi iliyopita, Rais Trump alisema Marekani itashambulia Iran iwapo italipiza kisasi kutokana na kifo cha Soleimani na kusambaratisha nchi hiyo kabisa.

Aliongeza kwamba Marekani ipo tayari kutekeleza mashambulizi makali katika makao 52 ya kitamaduni nchini Iran iwapo nchi hiyo ya Kiarabu itashambulia ubalozi wake au mali yake kwenye mataifa ya nje.

You can share this post!

Yaibuka ukafiri husukuma vijana kuua wazee

Ataka idhini aoe mke wa nduguye

adminleo