'Afufuka' siku yake ya kuzikwa
Na GEORGE MUNENE
HUZUNI iligeuka kuwa furaha Alhamisi katika kijiji cha Gitaugu, eneo la Mbeere Kusini, Kaunti ya Embu, baada ya mwanaume aliyedhaniwa kuaga dunia, na mwili wake kuhifadhiwa mochari, kupatikana akiwa hai hospitalini.
Familia ya mkulima mashuhuri wa ‘muguka’, Stephen Kivuti aliye na miaka 28, ilikuwa imekamilisha mipango yote ya kumpa mazishi ya heshima jana, lakini walipofika mochari kuchukua maiti yake kwa ajili ya kuizika, wakapata angali hai.
Bw Kivuti alianza kuugua Januari 2 mwaka huu na akakimbizwa hadi hospitali ya kaunti ndogo ya Kiritiri, ambako alilazwa akiwa amepoteza fahamu. Baadaye alihamishwa hadi Hospitali Kuu ya Kaunti ya Embu ambako alidaiwa kufariki.
Jambo lililofanya familia na wanakijiji kuamini kwamba alikuwa amekufa ni babake, James Nyaga wakati alipoenda hospitalini kumwona lakini akamkosa kwenye wodi, na hapo akaamua kuwa mwanawe alikuwa ameaga dunia.
Ripoti zinasema Mzee Nyaga alipomkosa mwanawe kwenye wodi alizirai, na alipopata fahamu wauguzi walikosa kumpa jibu kuhusu alikokuwa mtoto wake. Hapo ndipo alipojiamulia mwenyewe kwamba ameaga dunia.
“Nilipomkosa kitandani na wauguzi wakakosa kunijibu nilifahamu mwanangu hakuwa hai tena. Nilijua alikuwa maiti na sikuona haja ya kupoteza wakati ndipo nikaondoka kurudi nyumbani nikiwa na huzuni tele,” akasema Mzee Nyaga.
Mzee Nyaga alirudi nyumbani na kueleza familia yake, jamaa, marafiki na wanakijiji kuwa mwanawe amefariki na mipango ya mazishi ikaanza.
“Tulikusanya fedha za kununua jeneza, kuandaa vyakula vya waombolezaji na pia tukachapisha nakala ya kitabu chenye maelezo ya maisha ya marehemu na ratiba ya ibada ya mazishi,” akaongeza.
Hapo jana, watu wa familia walipofika kuchukua mwili wake mochari walishangazwa na maelezo ya wauguzi kuwa Bw Kivuti alikuwa akiendelea kupokea matibabu katika wodi.
Walielekea chumba hicho ambapo walimpata akiendelea kutibiwa.
“Tuna furaha kwamba mwana wetu ‘amefufuka’ na ataishi kwa muda mrefu,” mamake Bw Kivuti, Bi Frida Igoki akasema.
Nyumbani, hali ya kuomboleza ilibadilika na kuwa furaha jamaa na wanakijiji wakisheherekea uhai wa mtu waliyeamini wanasubiri mwili wake kuuzika.
“Mara ya kwanza tulibabaika hadi familia ikatueleza ukweli wa mambo. Huu ni muujiza kutoka kwa Mungu,” akasema Bw James Mitaru.
Chifu wa lokesheni hiyo, Josephat Nyaga alidhibitisha kwamba alikuwa ametoa kibali cha mazishi hayo: “Hata nilikuwa nikijitayarisha kuhudhuria mazishi hayo.”
Hospitali Kuu ya Kaunti ya Embu, kupitia afisa anayesimamia mochari, Paul Ngari, ilipuuzilia mbali madai ya “kufufuka” kwa Bw Kivuti.
“Hakuna mtu mwenye jina hilo ambaye mwili wake ulikuwa umehifadhiwa mochari. Madai kwamba alifufuka ni uongo kwa sababu Bw Kivuti hakuondoka kwenye wodi,” akasema Bw Ngari.
Afisa Mkuu Mtendaji wa hospitali hiyo, Dkt Daniel Mugendi alishtumu familia hiyo kwa kueneza habari za kifo cha Bw Kivuti kabla ya kupata thibitisho kutoka kwa hospitali.
“Familia yake haikumanika. Walienda kwenye wodi tofauti na wakamkosa ndiposa wakajiamulia alikuwa ameaga dunia. Wangepata maelezo zaidi kutoka kwa wahudumu wetu kabla ya kuandaa mazishi ya mtu akiwa hai,” akasema Dkt Mugendi.