• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
Msiwalazimishe wanafunzi waliofeli kurudia madarasa, walimu waonywa

Msiwalazimishe wanafunzi waliofeli kurudia madarasa, walimu waonywa

Na Waweru Wairimu

NAIBU Kamishna wa Kaunti ya Isiolo Mohammed Maow amewaonya wakuu wa shule dhidi ya kuwalazimisha wanafunzi kuyarudia madarasa yao kutokana na matokeo mabaya.

Bw Maow Alhamisi alisisitiza kwamba wanafunzi wote lazima wajiunge na madarasa mapya bila kujali iwapo walipita au la.

Aliongeza kwamba kuwalazimisha wanafunzi kurudia darasani kumesababisha baadhi yao kuacha shule na kuingia kwenye ndoa za mapema.

“Walimu wakuu hawafai kuwalazimisha wanafunzi warudie darasa. Badala yake, wanafaa waruhusiwe wajiunge na darasa linalofuatia bila kuzingatia kama walipita mtihani au la,” akasema Bw Maow.

Alifichua kwamba maafisa wake watakuwa wakizuru shule zote za umma kuangalia sajili ya wanafunzi ili kuhakikisha wote wapo na wamejiunga na madarasa yanayofuatia.

Afisa huyo ambaye pia alikuwa akizungumza mjini Isiolo pia aliwaomba wazazi waheshimu agizo lake litakalohakikisha serikali inatimiza lengo lake la wanafunzi wote kuwa shuleni.

Aidha alizitaka shule za kibinafsi pia kutowalazimisha wanafunzi kurudia darasa huku pia akiwaomba machifu kutembea nyumba hadi nyumba ili kuhakikisha wanafunzi waliofanya mtihani wa KCPE mwaka jana, wote wanajiunga na kidato cha kwanza.

“Wazazi lazima wahakikishe watoto wao wako shuleni na iwapo kuna masuala yanayoibuka, basi wanafaa kunifahamisha ili tuone jinsi ambavyo wanafunzi watasaidiwa kuendelea na masomo yao,” akasema.

Pia aliwaomba wazazi wafuatilie mienendo ya watoto wao kwa karibu ili kuwazuia kujiunga na makundi ya kigaidi au kuzamia matumizi ya dawa za kulevya.

Wakati uo huo Mkurugenzi wa Tume ya Kuwaajiri Walimu(TSC) Alex Cheruiyot amewaonya walimu wakuu dhidi ya kuwaruhusu walimu ambao hawako kwenye sajili ya elimu ya tume kufundisha kwenye shule zao.

You can share this post!

Masharti kwa wanachama wapya wa NHIF

KIKOLEZO: Ni zamu ya Bien na Chiki 2020?

adminleo