Habari

Lamu ni shwari na salama kwa uwekezaji – viongozi

January 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya Kaunti ya Lamu na ile ya kitaifa zinawarai wawekezaji kupuuzilia mbali matukio ya hivi majuzi ambapo eneo hilo lilikumbwa na mashambulio, na badala yake kuzuru Lamu na kuwekeza miradi mbalimbali.

Gavana wa Lamu, Fahim Twaha, Kamishna wa Kaunti hiyo Irungu Macharia na Kamanda wa Polisi eneo hilo, Muchangi Kioi, wamesema Lamu kwa sasa imedhibitiwa vilivyo kiusalama na kwamba wawekezaji, watalii na wanabiashara wengine wako huru kuzuru eneo hilo wakati wowote ili kuendeleza azma yao ya maendeleo.

Katika kikao cha jumla na wanahabari kwenye makao makuu ya Kaunti ya Lamu mjini Mokowe mnamo Jumatano, viongozi hao pia waliwataka wakazi eneo hilo kuondoa shaka na badala yake kuelekeza fikra zao katika kujiendeleza maishani.

Bw Twaha aliwashukuru walinda usalama kwa juhudi zao katika kuhakikisha amani na utulivu vinarejea eneo hilo.

Alisema serikali yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na idara ya usalama ili kuona kwamba amani na utulivu vinadumishwa Lamu.

Ningependa kuipongeza serikali yetu ya kitaifa, hasa wanajeshi wetu kwa juhudi zao katika kuleta amani eneo hili…

“Hakuna haja ya kujitia kiwewe au wasiwasi wowote. Lamu imedhibitiwa vilivyo. Kila mahali kunalindwa. Ningependa kuipongeza serikali yetu ya kitaifa, hasa wanajeshi wetu kwa juhudi zao katika kuleta amani eneo hili. Ningewasihi wawekezaji, watalii na wanamaendeleo wengine kuzuru eneo hili bila hofu. Lamu ni pahala patulivu na lazima kila mmoja ajivunie kuwa hapa,” akasema Bw Twaha.

Bw Macharia alisema maafisa wa kutosha wa usalama wamesambazwa kila eneo la Lamu ili kudhibiti usalama wa eneo hilo na kuwataka wakazi, wageni na watalii kutotishwa na yeyote.

Aliwasisitizia wale wenye nia ya kuendeleza miradi eneo hilo kufanya hivyo.

“Doria za walinda usalama zimeongezwa kote Lamu na msihofu. Wenye kuzuru Lamu kujivinjari au kuwekeza miradi yao nyote mnakaribishwe na mjisikie huru,” akasema Bw Macharia.

Naye Bw Kioi aliwataka wakazi kushirikiana vilivyo na walinda usalama eneo hilo ili kumaliza vita dhidi ya al-Shabaab na wahalifu wengine.