• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 4:01 PM
Wadai Kuria amekamatwa kwa kusema Miguna afaa kuruhusiwa nchini

Wadai Kuria amekamatwa kwa kusema Miguna afaa kuruhusiwa nchini

Na SAMMY WAWERU

WABUNGE wanaohusishwa na mrengo wa ‘Tangatanga’ sasa wanadai kukamatwa kwa mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria kunahusishwa na hatua yake kutetea wakili Miguna Miguna aruhusiwe kurejea nchini.

Mbunge huyo alikamatwa mapema Ijumaa na maafisa ambao hawakuwa na sare rasmi za polisi katika mkahawa mmoja jijini Nairobi kwa madai ya kumpiga mwanamke mmoja Desemba 2019.

Akizungumza nje ya kituo cha polisi cha Kilimani, Nairobi, ambako Kuria amezuiliwa, mbunge wa Kikuyu Bw Kimani Ichung’wa amesema mojawapo ya sababu zilizofanya Kuria akamatwe ni hatua yake kutetea Miguna arudi nchini.

“Kutetea Miguna Miguna aruhusiwe kurejea nchini tunaamini ni miongoni mwa sababu zake kukamatwa,” akasema Ichung’wa, kwa niaba ya wabunge wenza wa Tangatanga.

Alikuwa ameandamana na wabunge Mohammed Ali wa Nyali, Ndindi Nyoro (Kiharu), miongoni mwa wengine.

Mbunge huyo alisema Tangatanga haitababaishwa na yeyote katika kile alitaja kama “kueleza ukweli wa mambo”.

Ichung’wa akitoa ‘ujumbe wa Kuria’ alisema, “Kuria ameshikilia kwamba atabeba mzigo wa chochote kitakachoibuka kwa kusema ukweli”.

“Sote tunamuunga mkono na hatutababaishwa na yeyote kwa kusema ukweli. Huu ni mwaka wa kuambiana ukweli,” Bw Ichung’wa akasema.

Wiki hii, Kuria aliicharura serikali kwa kumkataza wakili Miguna kurudi nchini, akisema inakiuka haki zake kisheria.

Miguna alifurushwa nchini 2018 kwa kumuapisha kiongozi wa ODM Raila Odinga kama Rais wa Wananchi.

Wakili huyo ana uraia wa mataifa mawili; Kenya na Canada. Alipaswa kurejea nchini mapema wiki hii, lakini serikali ikatuma ilani kwa mashirika ya ndege aliyokata ada ya usafiri, dhidi ya kumsafirisha nchini. Miguna anahangaishwa licha ya mahakama kuu kuamuru aruhusiwe kurejea nchini.

Katika suala la kukamatwa kwa Kuria, mwanamke Joyce Wanja anadai Desemba 8 mwaka uliopita, mbunge huyo alimdhulumu baada ya kutofautiana kuhusu ripoti ya tume ya maridhiano ya BBI katika mdahalo ulioandaliwa na kituo kimoja cha runinga nchini.

You can share this post!

RIZIKI: Mitandao ya kijamii inavyomfaa kufanya mauzo ya...

Ibrahim Akasha ndani miaka 23

adminleo