• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Rungu la EACC laelekezwa kwa Ngilu

Rungu la EACC laelekezwa kwa Ngilu

Na BONIFACE MWANIKI

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) sasa imeelekeza macho yake kwa serikali ya Kaunti ya Kitui.

Imefichuka kuwa maafisa wawili wa ngazi za juu katika serikali hiyo inayoongozwa na Gavana Charity Ngilu, wamepangiwa kukamatwa wakati wowote sasa ili washtakiwe kwa kukiuka sheria za ununuzi wa bidhaa za umma.

Duru zilifichua kwamba mnamo wikendi, majasusi wa EACC walikuwa wakiwawinda afisa mkuu wa ununuzi bidhaa za umma katika kaunti hiyo, Bw Joshua Munyaka, na aliyekuwa kaimu afisa mkuu wa biashara, Bw Francis Keya.

Hii ni baada ya afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kukubali washtakiwe.

Bw Kea, ambaye kwa sasa ni mkurugenzi katika idara ya biashara ya mashirika, na Bw Munyaka wanakumbwa na madai ya ukiukaji wa sheria katika ununuzi wa malori matano yaliyotumiwa kusafirisha mifugo.

Hata hivyo, imesemekana wawili hao waliotarajiwa kukamatwa Ijumaa iliyopita walifahamu kuhusu mipango hiyo na wakakimbia mafichoni na kuzima simu zao za rununu.

Barua kutoka kwa afisi ya DPP iliyoandikwa Desemba 11, 2019 kwa Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, ilisema kuna ushahidi wa kutosha kufungua mashtaka ya uhalifu dhidi ya wawili hao.

Barua hiyo iliyoandikwa na naibu mkurugenzi wa mashtaka ya umma, Bi Emily Kamau, ilitumwa pia kwa wakili mkuu wa serikali katika Kaunti ya Kitui, Bw Bonny Okemwa.

Bw Okemwa aliruhusu mashtaka hayo yaendelee mbele Alhamisi iliyopita ndipo majasusi wa EACC wakaanza kuwasaka washukiwa hao wawili.

Seneta wa Kitui, Bw Enoch Wambua alisifu hatua hiyo ya EACC akasema amekuwa akipigania uwajibikaji wa matumizi ya mali ya umma katika kaunti hiyo kwa muda mrefu.

You can share this post!

Mabadiliko katika NHIF yapingwa vikali

Kamishna aonya walimu dhidi ya kutoza ada haramu za masomo

adminleo