• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
BBI yapasua nchi

BBI yapasua nchi

NA CECIL ODONGO

JUHUDI za kuwaunganisha Wakenya kupitia mchakato wa Jopo la Maridhiano (BBI) zimegeuka kinaya shughuli hiyo ikileta migawanyiko zaidi badala ya kupatanisha.

Walipoafikiana kushirikiana mnamo 2018, Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga walisema moja ya sababu ya handisheki ni kuwapatanisha Wakenya waliogawanyika kwa misingi ya kisiasa na kikabila.

Katika kile wawili hao walisema ni kufanikisha ajenda yao ya upatanisho, mwaka jana walibuni BBI ambayo ripoti yake Novemba.

Lakini ripoti hii imegeuka jukwaa la wanasiasa kuitumia katika mikakati yao ya uchaguzi wa 2022, badala ya kuweka mifumo ambayo itaweza kuwaleta wananchi pamoja.

Migawanyiko hii inachochewa zaidi na Bw Odinga na Naibu Rais William Ruto, ambao kila mmoja anapanga mikakati ya kujiweka katika nafasi bora ya kuchaguliwa kuongoza Kenya 2022.

Migawanyiko hii imeongezeka tangu wikendi iliyopita wakati mrengo wa kisiasa unaoongozwa na Bw Odinga ulipoanza kampeni za kupigia debe BBI, huku juhudi hizo zikipingwa na upande wa Dkt Ruto.

Kulingana na Bw Ruto, Bw Odinga na chama chake cha ODM wameteka shughuli ya BBI na wanaitumia kujiimarisha kwa ajili ya uchaguzi wa 2022.

Kulingana na Bw Gabriel Mutuma, ambaye ni mchanganuzi na mshauri kuhusu masuala ya uongozi, wanaounga mkono BBI wameonyesha wazi wanalenga kutimiza ajenda zao za kisiasa.

“Wanasiasa wanalenga kutumia BBI kuhakikisha wanaendelea kuwa uongozini hata baada ya 2022. Hofu ya Naibu Rais inatokana na jinsi washirika wake wanavyokandamizwa na hata amri za korti kupuuzwa,” akasema Bw Mutuma jana.

Lakini kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Profesa Hezron Mogambi, upande wa Naibu Rais umeonyesha unafiki kuhusu BBI kwa kuwa wanapinga mikakati yoyote wanayoiona itamzuia kushinda urais 2022.

“Kila mara uchaguzi unapokaribia, kila mtu hujiweka pazuri ili kuwa na ushawishi. Wandani wa Naibu Rais sasa wanaona BBI kama inayotumika kumzuia kuingia ikulu na ndiyo sababu wanasisitiza mikutano ya kupigia debe ripoti hiyo haina maana,” akasema Profesa Mugambi.

Naye mchanganuzi wa kisiasa Mark Bichachi anasema wandani wa Dkt Ruto hawataki ripoti hiyo itekelezwe kwa sababu itakuwa na nafasi kubwa ya kuamua mshindi wa 2022.

“Mnamo 2005 baada ya ushindi wa Raila na kundi lake la Orange kwenye kura ya maamuzi, kulikuwa na matumaini makubwa wangeshinda urais 2007, na hadi leo bado kuna imani walishinda uchaguzi huo. Hofu ya Dkt Ruto ni kwamba atakayedhibiti BBI ana nafasi nzuri ya kushinda 2022,” akasema Bw Bichachi.

Duru zinasema mrengo wa Bw Odinga, ambao pia unashirikisha pia Waziri wa Usalama, Fred Matiang’i na Katibu Karanja Kibicho unatumia kila mbinu ikiwemo kuwataka makamishna wa kaunti na maafisa wengine kuunga mkono BBI.

Pia kinara huyo wa ODM ameweza kuwashawishi wengi wa magavana kujiunga na kambi yake kwa ahadi ya vyeo akishinda urais 2022.

Kwa kufanya vikao katika maeneo tofauti, mrengo wa Bw Odinga unalenga kupiga vita vigogo wa siasa za maeneo hayo.

Mkutano wa kwanza uliandaliwa Kisii kwa kile wadadisi wanasema ni mbinu ya kuyeyusha ushawishi wa Dkt Ruto, ambaye alikuwa amepata uungwaji mkono wa wabunge wengi wa eneo hilo mwaka jana.

Mkutano mwingine umeandaliwa Kakamega wikendi hii ukilenga kufuta ushawishi wa Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetangula (Ford-Kenya). Magharibi mrengo huu una uungwaji mkono wa magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega), Wyclife Wangamati (Bungoma), Patrick Khaemba (Trans Nzoia) na Sospeter Ojamoong (Busia)

Mkutano pia umependekezwa Ukambani ukilenga kufuta ushawishi wa Kalonzo Musyoka eneo hilo kwa kutumia magavana Charity Ngilu (Kitui) na Kivutha Kibwana (Makueni).

Migawanyiko pia ipo katika eneo la Mlima Kenya ambapo magavana wengi hawajajitokeza wazi kueleza misimamo yao kuhusu BBI isipokuwa Anne Waiguru wa Kirinyaga ambaye yupo upande wa Bw Odinga.

You can share this post!

Trump aonya Iran dhidi ya kuua waandamanaji

UTEUZI: Tangatanga walia Uhuru alipendelea wandani wa Raila

adminleo