HabariSiasa

UTEUZI: Tangatanga walia Uhuru alipendelea wandani wa Raila

January 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa mrengo wa Tangatanga kutoka eneo la magharibi mwa Kenya wamelalamikia kile wanachotaja kama kupuuzwa kwa eneo hilo katika teuzi mpya ambazo Rais Uhuru Kenyatta alifanya serikalini Jumanne.

Walidai kwamba katika teuzi mpya ambazo kiongozi wa taifa alifanya, waliofaidi ni watu kutoka eneo la Nyanza ambao hawakumpigia kura kwa wingi katika uchaguzi mkuu wa 2017 walivyofanya watu kutoka eneo hilo.

“Japo watu wetu walipigia Jubilee kura kwa wingi kuliko wale wa Nyanza, tunasikitika kuwa Rais Kenyatta hajateua mtu kutoka jamii yetu ya magharibi katika orodha aliyosoma akiwa Mombasa. Ni watu wa Raila ndio wameteuliwa hawakumpigia kura uchaguzi uliopita,” Mbunge Sirisia John Waluke akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi,

Aliandama na wenzake Didmus Barasa (Kimilili), Dan Wanyama (Webuye Magharibi), Malulu Injendi (Malava) na kiranja wa wengi bunge Benjamin Washiali (Mumias Mashariki).

Katika mabadiliko ambayo Rais Kenyatta alitangaza Jumanne katika mawaziri, mawaziri wasaidizi na makatibu wa wizara, aliyekuwa Mbunge wa Nyakach Peter Odoyo aliteuliwa kuwa Waziri Msaidizi wa Ulinzi huku Afisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi wa Kuandaa Mitaala Nchini (KICD) Dkt Jwan Ouma akiteuliwa kuwa Katibu wa Wizara anayesimamia Mafunzo ya Kiufundi.

Bw Barasa alidai kuwa wawili hawa na watu wengine kutoka Nyanza, miongoni mwa wengine, waliteuliwa kwa sababu na ushawishi wa kiongozi wa ODM Raila Odinga kutokana na uhusiano wake wa karibu na Rais baada ya wawili hao kuridhiani kisiasa mnamo Machi 9, 2018.

“Hii handisheki kati ya Raila na Uhuru ndio sasa imepelekea watu wetu kukosa viti katika serikali hii ambayo tuliipigania kwa nguvu zetu zote. Rais hafai kutusahau ilihali ni sisi tulimsaidia wakati Raila na watu wake walisusia marudio ya uchaguzi Oktoba 26, 2017,” akasema.

Hata hivyo, Bw Washiali alikataa kuzungumzia suala hilo akisema Rais ana mamlaka ya kufanya mabadiliko na teuzi katika serikali yake anavyotaka.

“Nadhani Rais Kenyatta aliongozwa na busara katika mabadilika na teuzi aliyofanya leo (jana). Naamini walioteuliwa wataendeleza ajenda ya maendeleo ya Jubilee. Siwezi kumkosoa Rais kwa sababu ni bosi wangu,” akasema.

Wakati huo huo, wabunge hao wamekariri kuwa mkutano sambasamba ambao wamepanga kufanya mjini Mumias Januari 18 kujadili masuala ya ufufuzi wa sekta ya miwa utaendelea ulivyopangwa.

“Nimesikia watu fulani wakisema kuwa Mkutano wa BBI utakaofanyika mjini Kakamega siku hiyo ndio wa kipekee. Nawaambia kuwa sisi kama viongozi wanaojali masilahi ya wakulima wetu wa miwa tutakuwa mjini Mumiaa kujadili mustabali wao,” akasema Bw Washiali.