Habari Mseto

Taarifa za mashahidi 21 zakosekana kesi ya Kariuki

January 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ilifahamishwa Jumanne afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) haijamkabidhi bilionea Humphrey Kariuki nakala za ushahidi katika kesi inayomkabili ya ukwepaji kulipa ushuru wa Sh41bn kwa mamlaka ya kodi KRA.

Mawakili Kioko Kilukumi na Cecil Miller wanaomwakilisha Kariuki walimweleza hakimu mkuu mahakama ya Milimani Martha Mutuku kuwa ni miezi saba tangu bwanyenye huyo ashtakiwe na bado afisi ya DPP haijamkabidhi ushahidi ndipo aandae tetezi zake.

Bw Kilukumi alisema DPP aliwapa nakala yenye orodha ya mashahidi 28 lakini “wamepewa nakala za mashahidi saba tu.”

Wakili huyo alishangaa ushahidi wa mashahidi 21 uliko.

“Kutokana na tabia ya DPP kutotupa ushahidi ni vigumu kesi hii kutengewa siku ya kusikizwa kwa vile hatuwezi andaa tetezi za mashahidi bila kuona ushahidi uko namna gani,” Bw Kilukumi.

Aliomba mahakama iamuru DPP awakabidhi ushahidi ndipo wajiandae kuwakabili watakaofika kortini kutoa ushahidi dhidi yao.

Bw Kariuki aliyeshtakiwa Julai mwaka uliopita alikana mashtaka ya kukwepa kulipa ushuru wa Sh41bn.

Wakili Miller aliambia mahakama mamlaka ya ushuru KRA na maafisa wa Polisi kutoka afisi ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) walivamia kiwanda cha kutengeneza mvinyo cha Africa Spirits Limited (ASL) Januari 2019 na kukifunga.

“Yapata mwaka mmoja sasa tangu maafisa wa KRA na DCI kuvamia kiwanda cha ASL na kukifunga.Wafanya kazi zaidi ya 600 walipoteza kazi. Hata afisa wa Polisi alifia katika kiwanda hicho kilichoko mjini Thika,” alisema Miller.

Mbali na wafanyakazi kupoteza kazi na wamiliki wa kiwanda hicho kupata hasara ya mabilioni ya pesa kufuatia kufungwa kwa kiwanda hicho , Bw Miller alidokeza Serikali pia imepoteza zaidi ya Sh1.2bilioni za kodi.

Kila mwezi ASL na kiwanda cha Wow Beverages Limited (WBL) zilikuwa zinalipa kodi Sh150milioni kila mwezi.

Mahakama ilifahamishwa kuwa afisi ya DPP ilikuwa imeamriwa iwape washtakiwa nakala za ushahidi ifikapo Janauri 14, 2020 lakini “bado agizo hilo haijatekelezwa.”

Kiongozi wa mashtaka Vincent Monda akijibu alieleza mahakama washtakiwa walipewa ushahidi wote uliorekodiwa kwa njia ya elektronik.”

Lakini mawakili Kilukumi, Miller, Edward Oonge na Rubeen Dar walikubaliana kwamba “afisi ya DPP ilikaidi agizo la korti iwape nakala za ushahidi sio kwa njia ya elektronik ndipo wajiandae.”

Bw Kariuki ameshtakiwa pamoja na WBL na wakurugenzi wake Stuart Gerald Herd na Robert Thinji Muriithi, na ASL pamoja na wakurugenzi Peter Njenga Kuria na wakili Geoffrey Kaaria Kinoti Mbobua wamekabiliwa na mashtaka 21 ya kukwepa ushuru na kupatikana na risiti feki za ushuru wa forodha.

Washtakiwa wamekanusha mashtaka hayo na wako nje kwa dhamana.