Polisi wazima mkutano wa Mudavadi Mumias
SHABAN MAKOKHA na CHARLES WASONGA
POLISI wa Mumias wamefutilia mbali kibali ambacho walikuwa wametoa kwa makundi mawili yaliyopanga kufanya mikutano miwili katika uwanja wa Nabongo mjini Mumias Jumamosi hii.
Mikutano hiyo ilinuiwa kukinzani na ule wa uhamasisho kuhusu ripoti ya jopo la maridhiano (BBI) katika uwanja wa Bukhungu, mjini Kakamega na ambapo ulipangwa na Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya.
Mkutano wa Mumias uliopewa jina, “Western Region Development Consultative Forum” ulipangwa na kundi na wanasiasa wanaowaunga mkono kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula.
Kundi lingine likiongozwa na Seneta wa Kakamega Cleophas Malala pia lilikuwa limewasilisha ombi kwa polisi liruhusiwe kufanya maandamano katika eneo kunakokuzwa miwa la Mumias.
Kamanda wa Polisi katika kaunti ndogo ya Mumias Magharibi Peter Kattam alisema Kamati ya Usalama Wilayani (DSC) ndio alifikia uamuzi wa kufutilia mbali mikutano hiyo kutokana na “sababu za kiusalama”.
“DSC imeamua kufutilia mbali mikutano yote iliyopangiwa kufanyika na makundi mawili katika eneo hili la Mumias. Imethibitishwa kwamba makundi hayo mawili yana imani kinzani na huenda yakakabiliana,” akasema Kattam.
Alisema polisi wamewasiliana na waandalizi wa mikutano hiyo miwili kuhusu uamuzi wa kamati ya DSC na wametakiwa kuweka tarehe mpya ya mikutano yao.
“Tumewashauri wanachama wa makundi hayo mawili kutofika katika maeneo ya mikutano hiyo kuepusha uwezekano kuwa kutokea kwa mapigano,” Bw Kattam akaongeza.
Afisa huyo alisisitiza kuwa polisi hawataruhusu mkutano wowote kufanyika katika kaunti ya Kakamega kando na ule wa BBI ukatakaondaliwa katika uwanja wa Bukhungu.
Lakini mmoja wa waandalizi wa mkutano ambao ungefanyika uwanja wa Nabongo, waziri wa zamani Rashid Echesa alikashifu hatua ya polisi akisema kundi lake ndilo lilikuwa la kwanza kuomba kibali cha kufanya mkutano Mumias.