Orengo aanza kazi huku Wetang'ula akilia
Na VALENTINE OBARA
SENETA wa Siaya, Bw James Orengo, Jumatano ameanza kuchapa kazi kwenye afisi ya kiongozi wa wachache katika seneti huku Seneta wa Bungoma, Bw Moses Wetang’ula, ambaye ni mtangulizi wake akizidi kulalamikia jinsi alivyong’olewa kutoka kwa wadhifa huo.
Bw Orengo alichaguliwa na maseneta wa upinzani katika wadhifa huo baada ya madai kuwa Bw Wetang’ula hakuwa akiwahudumia ipasavyo.
Mwandani huyo wa Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, amekuwa akikutana na mabalozi mbalimbali afisini mwake.
Mnamo Jumanne, alikutana na Balozi wa Uingereza, Bw Nic Hailey, na jana akakutana na Naibu Balozi wa Australia, Bw Jonathan Ball.
“Tulijadiliana kuhusu hatua za kiuchumi na kisiasa, na umuhimu wa kudumisha uwiano,” akasema Bw Orengo.
Kwa kawaida mabalozi hukutana na viongozi mbalimbali wa bunge la taifa na wale wa seneti kwani asasi hizo mbili ndizo hutegemewa kupitisha sera na sheria ambazo hutoa mwongozo kuhusu jinsi taifa linavyoendeshwa.
Kufuatia ushirikiano wa Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga, mabunge hayo yatategemewa zaidi kupitisha sheria ambazo zitawezesha utekelezaji wa makubaliano yatakayofanywa na viongozi hao wawili kuhusu masuala tofauti yanayogusia uongozi na utendaji wa haki kwa wananchi.
Amponda Raila
Ingawa Bw Wetang’ula alisema hana haja tena na wadhifa huo wa kiongozi wa wachache, Jumatano alizidi kumshambulia Bw Odinga kwa madai kuwa ndiye alichochea maseneta kumtimua.
Alimtaka kinara huyo mwenzake wa NASA aondoke katika muungano ili ubaki chini yake na vinara wengine ambao ni Kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, na Bw Musalia Mudavadi anayeongoza Chama cha Amani National Congress (ANC).
“Ulifanya uamuzi wako ukasonga mbele na vuguvugu la NRM, kwani inafahamika huwa unabadilisha vyama katika kila uchaguzi,” akasema, kwenye mtandao wa Twitter.
Taarifa ya kwanza iliyotolewa na Bw Orengo kwa niaba ya maseneta wenzake ilitoa wito wa umoja na ushirikiano kutoka kwa seneta huyo wa Bungoma.
“Huu ni wakati wa siasa za maendeleo na ni lazima tuwe katika safari hii kwa pamoja kama taifa moja la Kenya,” akasema Bw Orengo.
Alitoa wito kwa viongozi waeke ubinafsi kando ili kupigania malengo ya kuleta haki uchaguzini, kulinda ugatuzi, mamlaka ya mahakama na sheria, kuleta usawa kitaifa, kupambana na ufisadi, kudumisha haki za binadamu na uongozi bora.