• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
Rais Kenyatta atangaza mikakati mipya ya kupambana na ugaidi nchini

Rais Kenyatta atangaza mikakati mipya ya kupambana na ugaidi nchini

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta ametangaza Ijumaa mikakati mipya ambayo serikali itatekeleza kufanikisha vita dhidi ya ugaidi nchini.

Mkakati huo utahusisha kuimarishwa kwa ushirikishi baina ya asasi mbalimbali za usalama, mafunzo, uimarishaji vifaa, ushirikishaji wa wanajamii na utoaji motisha kwa maafisa wa usalama.

Na kama njia ya kuwapa motisha maafa wa usalama, Rais Kenyatta ameamuru Tume ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu (SRC) kuhakikisha kuwa maafisa wanaohudumu katika maeneo ambayo hushuhudia mashambulio ya kigaidi kila mara wanalipwa marupurupu zaidi.

Maeneo hayo ni kama vile Kaskazini Mashariki na Pwani.

Rais pia ameamuru Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) kuwachunguza na kuwakamata wafadhili wa kundi la wapiganaji wa al-Shabaab kupitia biashara haramu.

“Njia zote ambazo adui hutumia kuchuma mapato kutoka Kenya kama vile biashara ya bidhaa zisizolipiwa ushuru sharti zikomeshwe. Hii ni kwa sababu shughuli kama hii ndiyo huwasaidia wafuasi wa al-Shabaab kupata fedha,” akasema.

Vilevile, Rais Kenyatta amewaamuru maafisa wa usalama kuanza operesheni kali ya kuwakomoa magaidi kutoka maficho yao katika eneo la Kaskazini Mashariki na Pwani ambayo yameathirika pakubwa.

Rais pia amemwamuru Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i ahakikishe kuwa maafisa wa polisi wanaofeli katika majukumu yao wanapigwa kalamu badala ya kuhamishwa kutoka kituo kimoja hadi kingine.

“Hatuwezi kuhamisha utendakazi mmbaya na kutoka kituo kimoja hadi kingine. Naamuru leo kwamba maafisa ambao watapatikana na makosa kama haya wafutwe kazi mara moja ili iwe funzo kwa wengine,” akasema.

Huku akikariri haja ya maafisa wa usalama kupewa silaha na mafunzo tosha, Rais Kenyatta ametoa wito kwa Makamishna wa Kaunti kufanikisha utekelezaji wa mipango ya kupambana na ugaidi katika kila kaunti.

“Na katika kufanya hivi, sharti wanajamii na wazee wahusishwe kikamilifu,” akasema Rais Kenyatta.

Vilevile, ameamuru ripoti kuhusu mafanikio katika utekelezaji wa mipango hiyo maarufu kama “Anti Terrorism County Action Plans” iwasilishwe kwake kufikia Agosti 2020.

Ameonya kwamba maafisa wa serikali ambao watafeli kufanya kazi kwa ushirikiano na wenzao katika vitengo vingine wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Rais amesema hayo siku chache baada ya wafuasi wa al-Shabaab kuwaua walimu watatu, ambao sio wenyeji, katika Kaunti ya Garissa.

Na mapema Januari maafisa wanne wa usalama waliuawa baada ya gari lao kulipuliwa na vilipuzi vya wavamizi kujitengenezea vilivyozikwa ardhini katika Kaunti ya Mandera.

  • Tags

You can share this post!

Seneti yaanza kusikiliza mashtaka ya kumtimua Trump

Baharia afariki, wawili waokolewa baada ya mashua kuzama...

adminleo