HabariSiasa

Hali yao mbaya

January 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

MAGAVANA sita, wabunge saba na seneta mmoja ni kati ya watu mashuhuri watakaopokonywa walinzi na bunduki wanazomiliki.

Hii ni baada ya serikali kuchukua hatua jana kuzima fahari ya ‘waheshimiwa’ wanaokumbwa na kesi za uhalifu mahakamani.

Mbali na ufisadi, inatarajiwa agizo hilo la polisi litagusia aina nyinginezo za uhalifu ikiwemo madai ya mauaji, kupigana na uchochezi.

Wengine wanaotarajiwa kuathirika na hatua hiyo ni matajiri washukiwa walio na bunduki na wanaokodisha polisi kuwapa ulinzi.

Idara ya Polisi jana iliamua Mkenya yeyote wa hadhi ya juu, ambaye ni mshukiwa wa uhalifu, atapokonywa walinzi na vile vile cheti chake cha kumiliki silaha kufutiliwa mbali.

“Idara ya Polisi hutarajia waheshimiwa wanaopewa huduma hizi za hadhi kujitolea kutii sheria kila wakati,” akasema Inspekta Jenerali wa Polisi. Hilary Mutyambai kupitia kwa taarifa iliyotolewa na msemaji wa polisi, Bw Charles Owino.

Hatua hiyo inamaanisha wahusika sasa watagharamia ulinzi wao kibinafsi.

Magavana ndio wamepata pigo kubwa kwani mbali na kupoteza walinzi na bunduki, pia wamekatazwa kuingia ofisini kutekeleza majukumu yao.

Magavana ambao wanatarajiwa kupokonywa ulinzi ni Mike Sonko (Nairobi), Ferdinand Waititu (Kiambu), Moses Lenolkulal (Samburu), Sospeter Ojamoong (Busia), Okoth Obado (Migori) na Stephen Sang (Nandi).

Pia Seneta Samson Cherargei wa Nandi yumo kwenye orodha hiyo.

Miongoni mwa wabunge kuna Babu Owino (Embakasi Mashariki), Moses Kuria (Gatundu Kusini), Rashid Kassim (Wajir Mashariki), Charles Njagua (Starehe), Aduma Owuor (Nyakach), David Gikaria (Nakuru Mjini Mashariki) na Stanley Muthama (Lamu Magharibi).

Agizo hilo lilitolewa siku ambayo Bw Owino alifikishwa mahakamani kuhusiana na madai ya kumpiga risasi na kumjeruhi Bw Felix Orinda almaarufu kama ‘DJ Evolve’ mnamo Ijumaa asubuhi.

Naye Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri Jumatatu alipokonywa bunduki yake kando na kuhojiwa na maafisa wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) mjini Nakuru kuhusiana na matamshi aliyotoa wiki iliyopita.

Bw Kuria naye alipokonywa walinzi wiki iliyopita, siku chache baada ya kukamatwa kwa madai ya kushambulia Bi Joyce Wanja katika kituo cha Royal Media mnamo Desemba.

Gavana Obado ana kesi kuhusu mauaji ya aliyekuwa mpenzi wake Sharon Otieno, ambaye alikuwa mja mzito wakati alipouawa.

Nao Sonko, Waititu, Ojamoong na Lenolkulal wanakabiliwa na kesi za ufisadi katika kaunti zao.

Gavana Sang naye alishtakiwa kwa madai ya uharibifu wa mali, uchochezi na utumizi mbaya wa mamlaka.

Seneta Cherargei pia alishtakiwa mwaka uliopita ikidaiwa alichochea jamii dhidi ya wale wasiomuunga mkono Naibu Rais William Ruto.

Bw Kasim naye ana kesi ya madai ya kumpiga Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Wajir, Bi Fatuma Gedi katika majengo ya bunge la taifa.

Wakati huo, Spika wa Bunge, Bw Justin Muturi alisema: “Bunge haliwezi kutumiwa kama maficho ya wahalifu.”

Bw Njagua almaarufu kama ‘Jaguar’ kwa upande wake alishtakiwa kwa kuchochea umma dhidi ya wafanyabiashara kutoka Tanzania.

Bw Gikaria alishtakiwa kwa madai ya utapeli katika umiliki wa ardhi, naye Bw Owuor akafikishwa mahakamani kwa madai ya kuhusika katika ufujaji pesa za umma alipofanya kazi katika Serikali ya Kaunti ya Nairobi ilipoongozwa na aliyekuwa Gavana Evans Kidero.

Bw Muthama alishtakiwa kwa madai ya kukwepa kulipa ushuru wa takriban Sh487 milioni.

Katibu Mkuu wa Chama cha ODM, Bw Edwin Sifuna jana alisisitiza kuwa chama chake hakiwezi kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya viongozi wanaokumbwa na kesi kama hizo, isipokuwa kama watapatikana na hatia mahakamani.